RAIS KIKWETE ATANGAZA NEEMA KWA MAJAJI NA MAHAKIMU



Serikali inatarajiwa kuajiri mahakimu wapya zaidi ya 300 katika mwaka ujao wa fedha 2014/ 2015 na mwaka unaofuata wa 2015 /2016, itaajiri mahakimu wengine 300. 
Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana jijini hapa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Kimataifa wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani.
Mbali na ajira hizo, Rais Kikwete pia alisema hivi karibuni anatarajia kuteua tena majaji 20 wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, pamoja na kujenga Mahakama Kuu katika mikoa minne ili kuendelea kuboresha Mahakama.
Alisema Serikali imejitahidi kuongeza rasilimaliwatu katika Mahakama, ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2005 kulikuwa na majaji 45, kati yao wanawake walikuwa 10, wakati sasa kuna majaji 78 na kati yao wanawake 30.
Hata hivyo, Rais Kikwete alieleza kwamba maboresho katika   Mahakama, hayawezi kufanikiwa, bila kushirikisha sekta nzima ya sheria.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwatahadharisha watoa haki mahakamani, kuacha kuegemea kuwapa au kutoa haki kwa watu wenye uwezo kiuchumi, hata kama haki hiyo, si yao. 
Alisema si busara kwa mhimili wa Mahakama, kutoa haki kwa watu wenye uwezo hususani kiuchumi huku wanyonge wakikosa haki hiyo. 
Pia, aliutaka mkutano huo, utumike kusaidia kuboresha shughuli za Mahakama ili zitoe haki sawa na kurekebisha sheria mbalimbali, zilizoridhiwa kutoka kwa Wakoloni ili sheria za Tanzania ziendane na mazingira ya nchi.   
Rais wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ), Jaji mstaafu Eusebia Munuo, alisema mkutano huo, utatoa fursa kwa majaji kubadilishana uzoefu, utakaosaidia katika utendaji wao wa kazi za kimahakama.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete alikwenda Kituo cha Uhamilishaji wa Mbegu Bora za Madume ya Ng’ombe kilichopo Usa River,  kujionea maendeleo ya kituo hicho na kuangalia ng’ombe aliyemtoa wiki moja iliyopita kwa kituo hicho kusaidia kutoa mbegu bora . 

No comments: