BOTI YAZAMA NA KUUA WATU WATANO ZIWA VICTORIAWatu watano wamekufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama ndani ya Ziwa Victoria.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, George Mayunga alisema ajali hiyo ilitokea Mei 23 mwaka huu saa 8 usiku. 
Boti ya Mv Kitoko II waliyokuwa wakisafiria kutoka Bugombe kupitia Kasenye kwenda Mganza wilayani Chato, ilizimika ghafla ikiwa katikati ya ziwa. 
Alisema boti hiyo inayomilikiwa na Mama Chacha aishiye Muganza , ilikuwa na abiria hao watano, ambao wote walikufa maji. 
Maiti aliyepatikana ni mfanyabiashara raia wa Rwanda, Jane Mlekatete (36) ambaye mwili wake ulikutwa ukielea. 
Wengine waliozama  ambao hawajapatikana ni Chikola Filbert (22) mkazi wa Muganza, Mapinduzi Daud ( 38 )mkazi wa Mwanza, Asha na Suzy waliotambuliwa kwa jina moja moja, wote wakazi wa Kasenyi na Mavombe (23) ambaye ni mkazi wa Muganza.
 Alisema chanzo cha ajali hiyo ni boti kubeba mzigo mkubwa. Kwa mujibu wa Kamanda, ilikuwa imebeba magunia 210.
Chanzo kingine cha ajali hiyo ni kwamba licha ya kubeba mzigo mkubwa, ilisafiri  usiku wakati kukiwa na upepo mkali na mawimbi yaliyosababisha injini ya boti hiyo kuzimika kabla ya kuzama.

No comments: