WALIOGOMA TAZARA KUKATWA MISHAHARA KUFIDIA HASARA



Mgomo wa wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia umesababisha hasara ya Sh bilioni 2.65 ambazo sasa Serikali imesema wafanyakazi watakatwa kwenye mishahara yao kufidia. 
Wafanyakazi hao ambao jana wametangaza kusitisha mgomo huo baada ya Mahakama kuubatilisha juzi, imeelezwa kwamba mishahara yao itakatwa kwa utaratibu utakaowekwa na Menejimenti. 
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Bunge mjini hapa, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe,   alisema mgomo huo ulioanza Mei 12 mwaka huu,  umesababisha  hasara ya dola za kimarekani milioni 1.6 sawa na Sh bilioni 2.65.
Awali, Dk Mwakyembe alitaka wafanyakazi hao kutii amri ya Mahakama kwa kurejea kazini na kusema atakayekaidi atakuwa amejifukuzisha. 
Aidha alisema Serikali itachukua hatua kali za kinidhamu kwa wafanyakazi na viongozi wa chama cha wafanyakazi watakaochochea migomo kinyume cha sheria ili kurejesha ufanisi katika mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi juzi ilitoa uamuzi kuwa mgomo huo ni batili na ikataka wafanyakazi  kurejea kazini baada ya Menejimenti kupeleka suala hilo kwenye Mahakama hiyo kupata ufumbuzi.
Alisema wafanyakazi hao kwa upande wa Tanzania  waligoma kinyume cha sheria kwa madai ya kutolipwa mishahara ya Februari kwa baadhi ya wafanyakazi pamoja na mishahara ya Machi na Aprili mwaka huu. 
Alisema Zambia wanaendelea na kazi licha ya kutolipwa kwa kutambua kuwa mapato ya mamlaka hiyo ni madogo ya dola milioni moja huku matumizi ikiwa dola milioni 2.5.
Mwakyembe alisema Mei 21 mwaka huu, Wizara iliagiza Menejimenti kuzungumza na wafanyakazi hao lakini waligoma kurejea kazini.
Baadaye Wizara ilizungumza na  uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli nchini (Trawu) na kukubaliana iwapo Serikali ingelipa mishahara ya Februari na Aprili wangerejea kazini kuanzia Mei 19 mwaka huu.
“Serikali ya Tanzania ilitimiza ahadi ya kulipa malimbikizo ya mishahara ya miezi hiyo kwa kuingiza fedha hizo katika akaunti ya Tazara  Mkoa wa Tanzania na baadhi ya wafanyakazi kuthibitisha kupokea fedha hizo,” alisema Dk Mwakyembe.
Hata hivyo alisema,  cha kushangaza baada ya kupokea fedha hizo wafanyakazi hao walianzisha madai mapya ya kutaka madaraka ya Mamlaka yarejeshwe kwenye mikoa  yaani ya Tanzania na Zambia na kutoa msimamo wa kutorejea kazini hadi yatakapotekelezwa. 
Waziri alisema kutokana na madai hayo, Menejimenti ya Tazara ilizungumza na uongozi wa Trawu na kuwaeleza kuwa suala hilo linahitaji uamuzi wa bodi kwa kuwa linahusu wanahisa wote wawili  jambo ambalo Trawu hawakukubaliana na ushauri huo. 
Menejimenti baada ya kuona kungetokea mgogoro wa kikazi, iliamua kupeleka suala hilo Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi ambayo imetoa uamuzi kwamba mgomo huo ni batili. 
Akizungumza jana Mwenyekiti wa Trawu, Kanda ya Dar es Salaam, Yusuph Mandai alisema wafanyakazi wamekubali kutii amri ya Mahakama na kurejea kazini kuanzia jana ingawaje hawajajua hatma yao.
Alisema  wamekubali kurudi kazini bila kujua hatma ya mishahara yao, ingawaje baadaye wataangalia ni kitu gani cha kufanya.
Kuhusu mgomo kusababisha hasara na kutakiwa kukatwa katika mishahara yao, alisema taarifa hiyo hawajaipata rasmi.
Hata hivyo kiongozi huyo wa wafanyakazi, alihoji, “Kama fedha hizo zinaweza kupatikana kwa kipindi cha mgomo pekee, kumbe wafanyakazi wangeweza kulipwa mishahara yao wanayoidai.”
Alisisitiza, “Tatizo letu kubwa ilikuwa ni kulipwa mishahara ambayo tulikuwa tunaidai…unajua hatulipwi kabisa na hata hatujui baada ya kukubali kutii amri ya Mahakama hatma yetu itakuwaje”, alisema Mandai.

No comments: