MTOTO WA BOKSI SASA AHAMISHIWA MUHIMBILIMtoto mwenye umri wa miaka minne aliyefungiwa ndani ya boksi kwa zaidi na miaka mitatu mkoani Morogoro, amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi na tiba zaidi huku wataalamu wakikuna vichwa namna ya kumrudishia afya yake. 
Imeelezwa jopo la madaktari  bingwa wa magonjwa mbalimbali ya binadamu wakiwemo wataalamu wa saikolojia, wanahitajika kwa ajili ya kumwezesha mtoto huyo mwenye ulemavu kuwa katika hali ya kawaida. 
Aidha, pamoja na uhitaji wa jopo la wataalamu hao, mtoto huyo ambaye amelazwa katika wadi ya watoto, atahamishiwa katika wadi maalumu ya watoto wenye utapiamlo  awe karibu na uangalizi wa lishe baada ya kubainika ana udhaifu mkubwa wa lishe.
Wakizungumza na mwandishi jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa Watoto wa MNH, Dk  Mwajuma Ahmada alisema  mtoto huyo hajazidiwa kuumwa.
Alisema walimpokea juzi usiku na hatua za awali zilizofanywa ni pamoja na kuchukua  baadhi ya vipimo kwa ajili ya uchunguzi.
“Mtoto aliletwa hapa jana (juzi) usiku, baadhi ya vipimo vimechukuliwa,  vingine atafanyiwa leo (jana) ikiwa ni pamoja na kumfanyia  huduma ya kum scan (kumwingiza kwenye mashine maalumu) mwili mzima ili tufahamu tatizo na tiba sahihi,” alisema Dk  Ahmada.
Alisema huduma ya tiba kwa mtoto huyo siyo ya daktari bingwa mmoja bali inahitaji jopo la wataalamu wakiwemo wa mifupa, saikolojia, viungo na magonjwa mbalimbali ya binadamu kumsaidia mtoto huyo.
“Kwa sasa hatuwezi kusema  lolote kubwa kuhusu mtoto huyo ndio kwanza kafika na ndiyo tuko kwenye hatua ya awali ya kuchukua vipimo, na leo atafanyiwa huduma ya kumulikwa mwili mzima ili tujue tunaanzia wapi”, alisema Dk Ahmada.
Alisema pamoja na kusubiri majibu ya vipimo, hatua wanayochukua ni ya kumhamishia kwenye wadi ya watoto wenye utapiamlo, ili kutibu maradhi hayo ambayo ndio yameonekana awali, kwani mtoto amekosa lishe na virutubisho muhimu vya awali.
Alifafanua, katika hatua hiyo ya awali, mtoto huyo atakuwa akipewa maziwa ya lishe na kuendelea na tiba ya dawa za kuua vijasumu kutokana na kusumbuliwa na vichomi. 
Akizungumzia kwa ufupi ikiwa mtoto huyo anaweza kurejea katika hali ya kawaida kwa viungo kunyooka na kutembea, Dk Ahmada alisema  pamoja na kusubiri majibu ya vipimo, lakini pia  tiba ya mtoto inategemea zaidi historia ya mtoto mwenyewe.
“Tiba ya huyu mtoto  inategemea pia historia halisi ya mtoto husika,  sasa hapa pana ugumu kwa kuwa mlezi wake wa sasa haifahamu historia vizuri ya mtoto, tunahitaji kuifahamu historia yake, mtoto alizaliwaje, hii ina maana kuwa je alizaliwa akiwa hana ulemavu wowote? Au ukuaji wake ulikuaje, sasa hatujapata mtu wa kutupa taarifa sahihi za mtoto”, alisema Dk Ahmada.
Alisema kitaalamu, mazingira ya kuishi tu ndani ya boksi bado hayatoi picha sahihi  ya athari za sasa za mtoto huyo alizopata, na kwamba zipo sababu za kufahamu historia  hasa ya undani ya mtoto huyo iweze kutoa dira kwa wataalamu wa tiba hospitalini hapo.
Alisema pamoja na kwamba mtoto huyo atapatiwa tiba, lakini bado athari zitabaki za ukuaji wake. Alifafanua kwamba kwa hali ya sasa, kimo chake na  kutotembea haviendani na umri wake. 
Aliongeza, baada ya vipimo kutokana na tatizo kujulikana watafahamu wapi pa kuanzia  na hilo litafanywa kwa ushirikiano wa jopo hilo la wataalamu na kwamba anaamini tiba sahihi itarejesha afya ya mtoto huyo.
Kwa upande wake, Ofisa Muuguzi Mwandamizi wa Wadi B ya watoto hospitalini hapo, Clara Nahum, alisema hali ya mtoto siyo mbaya ila ana utapiamlo uliokithiri.
Muuguzi huyo alisema, hali ya mtoto inaonesha alikosa huduma muhimu ikiwemo virutubisho muhimu vilivyohitajika wakati wa makuzi ya awali.
“Amekosa mahitaji muhimu yakiwemo madini na hata madini ya mwanga, hivi sasa tunamtibu vichomi na bado anaendelea kuchukuliwa vipimo na majibu yakitoka madaktari watajua wapi pa kuanzia, ila tunamhamishia wodi ya watoto wenye utapiamlo “, alisema Nahum.
Alisema katika wadi hiyo kuna wataalamu wa lishe ambao wanafahamu watoto wenye maradhi hayo jinsi ya kuwatibu kwa kutumia vyakula lishe vinavyotolewa kulingana na hali ya mtoto ilivyo.
Kwa upande wake, mlezi wa mtoto huyo , Josephina Joel akizungumza na gazeti hili wadini hapo alisema mtoto  anaendelea vizuri ingawa juzi alikuwa na homa. Hata hivyo alisema imeshuka, na kwamba kadri siku zinavyosonga, anaona uchangamfu wa mtoto.
“Tulifika hapa juzi usiku, tulitoka Morogoro na gari ya wagonjwa saa 11, jioni tukafika hapa saa tatu usiku tukapokewa na mtoto akafanyiwa baadhi ya vipimo ndipo tukaletwa wodini saa saba usiku, nilikuwa nimechoka nikalala, mtoto akawa ananiamsha, mama usilale amka tucheze, ila baadaye naye akalala”, alisema Josephina.
Alisema mtoto bado ana woga wa mwanga kwani usiku ili alale anataka taa izimwe na wakati mwingine bado anaogopa watu na kukataa wasimbebe na kuongeza akiwa anambeba mara nyingine hulalamika anaumia viungo.
Mwandishi wa habari hizi, alizungumza na mtoto huyo katika mahojiano mafupi:  
Mwandishi: Unaitwa nani mtoto mzuri?
Mtoto : Akataja jina lake
Mwandishi :Utakula nini?
Mtoto:Chipsi (viazi vya kukaanga)
Mwandishi:Njoo nikubebe
Mtoto:Sitaki naumia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Morogoro, Mganga Mkuu Mfawidhi wa Mkoa Morogoro,   Rita Lyamuya alisema mtoto huyo amepelekwa Muhimbili kwa ajili uchunguzi zaidi hasa kwa upande wa mifupa.
Alisema kwa kuwa juzi kulikuwa na wagonjwa wengine ambao walipewa rufaa ya kwenda hospitalini hapo, uongozi uliona ni vyema pia mtoto huyo aingizwe kwenye msafara huo  badala ya kusubiri jana kama ilivyokuwa imepangwa. 
“Hatukuona haja ya kusubiri mpaka asubuhi wakati gari tayari limepatikana kuna wagonjwa ambao wamepangiwa kwenda huko,” alisema
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu alisema juzi walipofika hospitalini mkoani humo kwa ajili ya kumjulia hali mtoto huyo na kukuta wauguzi wakimhangaikia huku akiwa analia, iliwafanya washituke na kudhani kuwa  amezidiwa.
Mtoto huyo alikuwa akiishi na wanandoa Mariamu Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30) ambao juzi walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kula njama na kutenda ukatili kwa mtoto huyo. Pia baba yake mzazi, Rashid Mvungi (47) mkazi wa Lukobe alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka hayo. 

No comments: