Benki
ya BOA Tanzania imeanza kutoa mikopo ya riba nafuu kwa sekta ya afya, ili
kuwezesha zahanati, vituo vya afya na hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.
Meneja
Mwandamizi wa Masoko wa benki hiyo, Solomoni Haule, aliwaambia waandishi
wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa, mikopo hiyo itawezesha
sekta hiyo kutoa huduma bora kwa jamii.
“Benki
imeanza kutoa mikopo kwa sekta ya afya, ili kuwezesha sekta hiyo muhimu kutoa
huduma bora na kuleta maendeleo,” alisema.
Alisema
huduma hiyo ya mikopo inayoitwa Tiba Finance, iliyoanza kutolewa Aprili mwaka
huu, ni ya riba nafuu na inatolewa kwa muda mfupi na muda mrefu
unaokwenda hadi miaka minne.
Alisema
benki inaamini kuwa changamoto kubwa zinazokabili sekta hiyo kama vitendea
kazi, mashine za kisasa, kujenga na kukarabati majengo, na dawa za kutosha,
vinaweza kupungua na kuisha kabisa kutokana na huduma za mikopo hiyo.
“Kupitia
mikopo hii, tunaamini watamaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto
hizi,” alisema.
Alisema
katika kufanikisha azma hiyo, benki inashirikiana na asasi ya Medical Credit
Fund, kujengea uwezo taasisi hizo, ili zitoe huduma bora.
“Tumejipanga
kwa kushirikiana na asasi hii kwenda katika kila taasisi itakayokopa kutoa
elimu. Tutafundisha namna ya kutumia vifaa vya kisasa vya kitabibu, mazingira
ya kazi, utendaji na kutengeneza mipango ya mahesabu ya kibiashara,” alisema.
Alisema
benki hiyo yenye matawi katika mikoa ya Dar es Salaam (10) na matawi
mengine Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mtibwa, Mbeya, Tunduma, Mwanza, Kahama
na sasa Mtwara, ilishawapatia semina wafanyakazi wake kutoa mikopo kwa
sekta hiyo ya afya.
No comments:
Post a Comment