BALOZI WA MISRI AIPA MUHIMBILI VIFAA VYA MILIONI 400Balozi wa Misri nchini ametoa msaada wa vifaa vya upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili vyenye thamani ya Sh  milioni 400.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela, alisema hayo katika hafla fupi ya kupokea vifaa hivyo iliyofanyika hospitalini hapo.
Alisema msaada wa vifaa hivyo, umefika wakati muafaka ambapo Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatekeleza mkakati wa kuboresha na kuimarisha huduma za afya. 
Aliongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia wagonjwa hasa wale wanaoandaliwa kwenda kufanyiwa upasuaji walioko chumba cha upasuaji na wale wanaohitaji uangalizi maalumu baada ya kufanyiwa upasuaji.
Pia alisema katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya upasuaji ni wenye matatizo ya urolojia kwa hiyo huduma hii ni muhimu sana hapa nchini.
Huduma ya urolojia hapa nchini inatolewa na baadhi ya hospitali za rufaaa lakini idadi kubwa ya Wagonjwa wanaohitaji huduma hizo hupata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya  Rufaa ya KCMC iliyopo Mkoani Kilimanjaro. 
“Katika Hospitali ya Muhimbili urolojia ilianzishwa rasmi mwaka 2008 chini ya Idara ya Upasuaji lengo ni ni kuboresha huduma kwa wananchi” alisema Njelekela.
Alisema huduma ambazo zimekuwa zikitolewa na kitengo cha urolojia ni pamoja na uvimbe wa tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo kutokana na kovu, saratani ya kibofu,saratani ya tezi la kiume na mawe kwenye figo.
Aidha aliishikuru serikali  serikali ya Misri kwa ushirikiano wake mkubwa na Tanzania kwani wamekuwa wakipokea wataalamu kuja kukaa na wataalamu hapa nchini ili kuwapa ujuzi zaidikatika maeneo mbalimabli ya huduma za kibingwana urolojia pia aliomba urafiki huu na ushirikiano huu uzidi kuimarishwa siku hadi siku.
Naye balozi wa Misri nchini, Hossam Moharam alisema wataendelea kuisaidia Muhimbili kwa kuipatia vifaa tiba mbalimbali vya upasuaji na pia tutaendelea kubadilishana uzoefu.
“Uhusiano wetu ni wa muda mrefu na tutaendelea kushirikiana na kushikamana ili tuweze kusaidia jamii na tutahakikisha tunaendelea kubadilishana ujuzi” alisema Moharam.

No comments: