BENKI YAZINDUA TAWI SOKONI KARIAKOO



Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam limepongezwa kwa kukuza uchumi nchini, kutokana na kupokea wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi  Mkuu wa Benki ya FNB Tanzania, Dave Aitken alisema hayo  Dar es Salaam  jana wakati akizindua tawi jipya la benki hiyo.
Alisema ingawa ni wachangiaji ipo haja ya  taasisi za fedha kuwafikia wajasiriamali wengi.
Alisema wafanyabiashara wengi wa soko hilo wana mikakati mikubwa ya kuvutia bidhaa zao, jambo linalosababisha wafanyabiashara kutoka nchi zisizokuwa na bahari kufika na kujipatia bidhaa.
Kariakoo ni eneo ambalo wanafika wafanyabiashara kutoka nchi zisizokuwa na bahari, ambapo kutokana na shughuli za biashara, husaidia kukuza  uchumi wa nchi.
Kuhusu tawi  hilo, alisema lengo la benki hiyo ni kuwa mstari wa mbele katika kukuza sekta za fedha, kwani  ina mpango wa kuleta wataalamu kutoka Ukanda wa Jangwa la Sahara katika sekta ya kilimo na madini, ambao watakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu, Andy Watkins, alisema uchumi wa Tanzania umekuwa kwa asilimia 7, ukilinganisha na miaka iliyopita.
Alisema ongezeko hilo, limetokana na shughuli mbalimbali, kama vile uchimbaji wa madini, utalii, viwanda na kilimo.
Alisema Kariakoo ni kitovu cha biashara, ambapo waingizaji na wasambazaji hutumia soko hilo, kufanya biashara zao, hivyo huduma za kibenki zitaimarisha maendeleo yao katika ngazi ya mtu mmoja mmoja.

No comments: