BARAZA LA WAWAKILISHI LACHELEWA KUANZA VIKAO VYAKEBaraza la Wawakilishi lililazimika jana kuahirisha kwa muda kikao chake,  baada ya wajumbe wengi kuchelewa na hivyo kuwepo idadi ndogo ya watu 17.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ali Abdalla Ali aliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kutimiza majukumu yao, ikiwemo kuhudhuria bila ya kuchelewa katika vikao vya baraza hilo. 
“Waheshimiwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nawakumbusheni majukumu yenu ikiwemo kuhudhuria vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa wakati ili kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa katiba ya kuwahudumia wananchi,” alisema.
Naibu Spika alilazimika kuahirisha kikao asubuhi na kusubiri wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa muda wa dakika tano hadi walipotimia idadi ya wajumbe 40, ambayo ndiyo inayokubalika kwa ajili ya kuanza vikao vya baraza.
Akizungumza na mwandishi, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamadi alisema kukosekana kwa kanuni zinazotoa adhabu kwa wajumbe katika suala la kuchelewa kwa vikao ni moja ya kasoro kubwa katika kuendesha vikao vya Baraza la Wawakilishi.
“Hayo ni mazoea kwa wajumbe kwa sababu hakuna kanuni zinazowabana na kutoa adhabu kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kukabiliana na tatizo la kuchelewa kuhudhuria vikao hivyo...ndiyo maana tatizo la kuchelewa lipo mara kwa mara,” alisema.
Mmoja ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, alisema wajumbe wengi kutoka CUF wapo kisiwani Pemba, wakishiriki katika chaguzi mbali mbali zinazofanyika katika ngazi ya chama hicho.

No comments: