WAZIRI ASEMA HAKUNA TATIZO WABUNGE KUOMBA FEDHA LAPF


Imeelezwa kuwa suala la wabunge na mawaziri kuomba fedha kwa ajili ya maendeleo katika majimbo yao kwenye mifuko ya jamii na taasisi nyingine  siyo baya, kwani wana fungu maalumu kwa ajili hiyo.Pia imeelezwa kuwa mbaya ni kukopa katika mifuko ya jamii na kushindwa kulipa, huku kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe akitajwa kukopa na sasa ana hati ya kukamatwa kutokana na tukio hilo.Suala hilo liliibuka bungeni jana baada ya Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM) kuomba mwongozo kwa naibu spika kutokana na Mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kutaja majina ya wabunge na mawaziri kuomba fedha katika Mfuko wa Hifadhi za  Jamii wa Serikali za mitaa (LAPF).Komba alikanusha kupokea fedha hizo kwani hajui hata ofisi za mfuko huo zilipo isipokuwa ni taasisi ya Nyasa Development Fund ambayo yeye ni mlezi ndiyo waliomba fedha hizo na kumtaka Lissu kukanusha au kuomba radhi.Baada ya mwongozo huo, Waziri katika ofisi ya Makamu wa Rais, Sera , Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisimama kwa niaba ya serikali na kusema kuomba fedha siyo jambo la ajabu, kwani kuna fungu maalumu kwa ajili hiyo kusaidia shughuli za maendeleo kwa jamii. 
Lukuvi alisema hata yeye aliishaomba katika mfuko mmoja fedha na kupewa milioni tatu kwa ajili ya shule ya Idodi iliyoungua moto na kusababisha vifo kwa wanafunzi.Lukuvi aliungwa mkono na Waziri wa Kazi na Ajira anayesimamia mifuko hiyo ya hifadhi za jamii, Gaudentia Kabaka aliyesema mifuko hiyo inaruhusiwa kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya jamii.Akijibu hoja ya fedha hizo kupewa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee, alisema siyo kweli na dhahiri mtu hawezi kupewa kitu ambacho hajaomba hivyo inawezekana wabunge wa upinzani hawakuomba.“Mheshimiwa Lukuvi yuko sahihi kwani mifuko hiyo inaruhusiwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya masuala ya Elimu, Afya na kiuchumi kwani wana fungu maalumu kwa ajili hiyo, hata taasisi kama mabenki wanasaidia katika masuala mbalimbali,”alisema.“Wapo wabunge waliokopa katika mfuko wa NSSF wana arrest warrant ingawa ni mambo binafsi acha, lakini hawajarudisha kwa muda mrefu hayo ndiyo makosa kwa sababu ni mambo yao binafsi,” alisisitiza.Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia alimtaka Lissu kama ana ushahidi kuuweka mezani huku akimshangaa Lissu  kwa madai hayo wakati kiongozi wake Mbowe anadaiwa mkopo hajalipa kwa muda mrefu.Akijibu hoja hizo, Lissu alidai mfuko huo wa LAPF unatoa kwa wabunge wa CCM pekee na kudai itasababisha kushindwa kusimamia taasisi hizo kutokana na mgongano wa kimaslahi.Akizungumzia suala hilo, Naibu Spika Job Ndugai alisema wabunge wanatakiwa kutoa hoja kwa utulivu bila kurushiana maneno  huku wakijichunguza kwanza bila kujiona ni salama kwani itarudi kwako.Akimjibu Lissu baada ya kumtaja ni mmoja wa waliochukua fedha hizo, Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) aliomba mwongozo kwa Spika kwa Lissu kuzungumzia suala hilo kwa maslahi binafsi kutokana na kuwa anamtetea mahakamani mfanyakazi wa LAPF aliyefukuzwa kazi kwa kufuja fedha za mfuko huo.Alisema anatuhumu  wabunge kuomba fedha kwa maendeleo ya majimbo huku akimtetea aliyefuja fedha za wanachama  huku akiahidi kutafuta fedha katika taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuweka umeme kwenye jimbo la Lissu ambalo ni kijiji kimoja tu ndiyo chenye umeme.

No comments: