BAJETI WIZARA YA HABARI MICHEZO NA UTAMADUNI

HOTUBA YA WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO, MHE. DKT. FENELLA E. MUKANGARA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/2015


A.            UTANGULIZI

1.                  Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo kwenye Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii sasa naomba kutoa hoja ya kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Asasi zake kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015.

2.                  Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda na kunipa nguvu ya kutekeleza majukumu yangu na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha bajeti hii.

3.                  Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima nitumie fursa hii kuwapongeza Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa uongozi wao thabiti ambao umeendelea kudumisha amani na mshikamano wa Taifa letu. Tunajivunia pia matunda ya Waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao mwaka 2014 umetimiza miaka 50. Uongozi wao umetuwezesha kufikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa tuliyonayo hivi sasa.

4.                  Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb.), kwa kazi nzuri wanazozifanya za ujenzi wa nchi yetu. Aidha, nikushukuru wewe binafsi Mhe. Spika, Mhe. Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mnaonipa ambao unaniwezesha kutekeleza kikamilifu majukumu niliyokabidhiwa ya kulitumikia Taifa letu.

5.                  Mheshimiwa Spika, katika maandalizi  ya hotuba hii, Wizara imezingatia maudhui yaliyotolewa katika Bunge lako Tukufu kupitia Hotuba ya  Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, hotuba yangu imezingatia pia maelekezo na malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/2015.

6.                  Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya uongozi yaliyotokea, natumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote walioteuliwa kuongoza Wizara mbalimbali.  

7.                  Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kujadili, kuchambua na kuboresha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni matumaini yangu kuwa baada ya kukamilika wananchi watapata fursa ya kupiga kura za maoni kama ilivyopangwa ili Taifa letu liweze kupata Katiba Mpya iliyo bora.

8.     Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuwapongeza wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuishauri Wizara katika maeneo mbalimbali. Wizara itaendelea kuzingatia na kutekeleza ushauri unaotolewa. Shukrani na pongezi zangu ziende kwa viongozi wapya waliochaguliwa kuongoza Kamati hii yaani, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Saidi Mtanda (Mb.) na Makamu Mwenyekiti, Mhe. John Damiano Komba (Mb.). Nawapongeza pia wajumbe walioteuliwa kuunda Kamati hii. Ushauri wao ndio umefanikisha maandalizi ya hotuba hii.

9.     Mheshimiwa Spika, napenda  kumshukuru aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mhe. Jenista Joachim Mhagama (Mb.), kwa kazi nzuri aliyoifanya katika Kamati hii.

10.  Mheshimiwa Spika, napenda kutoa pongezi kwa Wabunge wapya waliochaguliwa hivi karibuni kwa ushindi wa kishindo ambao ni Mhe. Yusuf Salim Hussein, (Mbunge wa Chambani), Godfrey William Mgimwa, (Mbunge wa Jimbo la Kalenga) na Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, (Mbunge wa Jimbo la Chalinze).

11.  Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawapongeza wanahabari pamoja na wadau wote wa sekta ya habari kwa kazi nzuri ya kutoa habari na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuuelimisha umma wa Watanzania. Aidha, napenda kutambua mchango mkubwa wa vijana wote katika kuinua  uchumi kwa kuwa wao ni takriban asilimia 70 ya nguvu kazi ya Taifa letu. Vilevile, niwapongeze wanamichezo wote ambao wameshiriki katika kuliletea heshima taifa kupitia mashindano ya michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Kwa namna ya pekee nachukua fursa hii, kutoa pongezi za dhati kwa Timu ya Mpira wa Miguu ya Watoto wanaoishi katika mazingira magumu kutoka Mkoa wa  Mwanza iliyotwaa Kombe la Dunia la Watoto wa Mitaani nchini Brazili. Hali kadhalika nawapongeza kwa dhati kabisa wasanii wote ambao wamekuwa kioo cha jamii katika kulitangaza taifa letu ndani na nje ya nchi yetu.  Nawapongeza hasa kwa jinsi walivyoshiriki kikamilifu katika kuhamasisha jamii kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.

12.  Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa familia na wananchi wa Jimbo la Kalenga na Jimbo la Chalinze kwa kuondokewa na Wabunge wao, Marehemu William Augustao Mgimwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, ambaye  alifariki tarehe 01 Januari 2014 nchini Afrika Kusini na Marehemu Said Ramadhani Bwanamdogo aliyefariki tarehe 22 Januari 2014. Aidha, ninawapa pole Watanzania wote waliopoteza ndugu zao kutokana na ajali, majanga na maradhi mbalimbali. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi, Amina!

13.  Mheshimiwa Spika, hotuba yangu imegawanyika katika maeneo makuu matano kama ifuatavyo: eneo la kwanza ni Utangulizi, eneo la pili ni Majukumu ya Wizara,  eneo la tatu linahusu Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2013/2014, eneo la nne linahusu Mpango na Bajeti kwa mwaka 2014/2015 na eneo la tano ni Hitimisho.

B.      MAJUKUMU YA WIZARA

14.                   Mheshimiwa Spika, Wizara inatekeleza majukumu ya msingi yafuatayo:-
i)     Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera za Sekta za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo;
ii)   Kuratibu na kusimamia masuala ya maendeleo ya vijana ili kuwawezesha kujiajiri, kuajirika na kujitegemea;
iii)  Kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali na kusimamia vyombo vya habari  nchini;
iv)  Kuratibu na kusimamia maendeleo ya utamaduni nchini; 
v)    Kuratibu na kusimamia maendeleo ya michezo nchini;
vi)  Kusimamia utendaji kazi wa Asasi, miradi na programu zilizo chini ya Wizara na
vii)   Kuendeleza, kuwezesha na kuratibu masuala ya kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara.

C.   MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI  KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014

Mapato na Matumizi

15.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya Shilingi 882,203,000 kutoka vyanzo mbalimbali. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2014 jumla ya Shilingi 663,029,569 zilikusanywa ambazo ni sawa na asilimia 75 ya lengo la makusanyo kwa mwaka.  Mchanganuo wa makusanyo upo kwenye  Kiambatisho Na. I.

16.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi  17,628,045,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Fedha hizo zilijumuisha Mishahara shilingi 9,257,125,000 (Wizara ni Shilingi 2,617,598,000 na Asasi ni Shilingi 6,639,527,000). Matumizi Mengineyo (OC) shilingi 8,370,920,000 (Wizara ni Shilingi 4,941,920,000 na Asasi ni Shilingi 3,429,000,000). Hadi mwezi Aprili, 2014 jumla ya Shilingi 13,292,539,498 za Matumizi ya Kawaida zilipokelewa na kutumika ambapo kati ya fedha hizo Matumizi Mengineyo ni Shilingi 4,740,957,000 na Mishahara ni Shilingi 8,551,582,498.

Miradi ya Maendeleo

17.              Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara ilitengewa jumla ya Shilingi 12,700,000,000 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2014 jumla ya Shilingi 4,327,500,000 zilipokelewa ambazo ni sawa na asilimia 34 na Shilingi 2,310,021,000 zilitumika. Miradi iliyotekelezwa ni pamoja na Upanuzi wa Usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ujenzi wa Ofisi - BAKITA, Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.


SEKTA YA HABARI

18.           Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea na utendaji wa kazi zake huku ikikabiliana na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni baadhi ya vyombo vya habari kukiuka sheria  kwa kuandika na kutangaza habari ambazo hazizingatii kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari. Aidha, kuongezeka kwa mifumo na njia za mawasiliano kama mitandao ya kijamii kwenye “internet” kumeathiri maudhui ya habari zinazotolewa. 

19.           Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hizo, Wizara imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana nazo, zikiwemo kutoa onyo na kufungia baadhi ya vyombo vya habari vilivyokiuka maadili. Wizara pia imeelekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutekeleza kikamilifu mpango wa kusajili wamiliki wote wa mitandao hiyo. Vilevile, Wizara inaendelea kutoa elimu na kuwaelekeza wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.20.             Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara imekamilisha maandalizi ya Muswada wa Sheria ya kusimamia Vyombo vya Habari na sasa uko katika hatua nzuri.  Kwa kuzingatia utaratibu uliopo, Muswada huu utafikishwa katika Bunge lako Tukufu lijalo la kutunga Sheria.


21.             Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuimarisha njia za mawasiliano kati ya Serikali na Wananchi wake, Wizara inafanya maboresho ya Tovuti ya Wananchi ili kuweza kuimarisha mifumo na monekano wa Tovuti hiyo. Maboresho hayo yakikamilika, yatawawezesha Wananchi popote walipo                                                                      kuwasiliana na Serikali kwa kutumia njia za kisasa. Aidha itawapunguzia wananchi  gharama za kuwasilisha kero, hoja na maoni mbalimbali katika Taasisi za Serikali. Kazi ya kuijenga upya na kuimarisha Tovuti hiyo ili kuwa na muonekano mpya unaokidhi mabadiliko ya sasa ya Sayansi na Teknolojia inatarajiwa kukamilishwa mwisho wa mwaka  wa fedha 2013/2014.

22.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kukusanya habari, kupiga picha za matukio mbalimbali ya Serikali na kuzihifadhi katika maktaba; pamoja na kuzisambaza kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kutoa habari na kuelimisha jamii. Wizara kama Msemaji Mkuu wa Serikali, ilifafanua masuala na hoja mbalimbali zinazohusu Serikali.

23.              Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia Vitengo vya Mawasiliano Serikalini kwa lengo la kutoa habari na kuelimisha umma juu ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Wizara imetoa mwongozo ulioainisha taratibu za kuendesha Vitengo hivyo na kuhimiza Wizara na Asasi zote za umma kuajiri Maafisa Mawasiliano Serikalini. Hali kadhalika, Wizara imeratibu jumla ya mikutano 255 ya wasemaji wa Asasi za Serikali na Vyombo vya Habari. Mikutano hii imesaidia kuwaelimisha Wananchi kuhusu shughuli za Serikali zinazofanyika kwa maendeleo yao.

24.             Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kuratibu ushiriki wa vyombo vya habari katika vikao vya Bunge vilivyofanyika Dodoma na pia kuhakikisha inawapatia vitambulisho waandishi wa habari wa ndani na nje wenye sifa za taaluma ya uandishi wa habari.

25.             Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia  kupitia TCRA, ilikamilisha awamu ya kwanza ya uhamaji wa kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analoji kwenda dijiti.  Baada ya zoezi hili tathmini imefanyika ambayo ilionesha mwitikio mzuri wenye mafanikio.  Hivi sasa zoezi hili limeingia katika awamu ya pili iliyoanza tarehe 31 Machi 2014. Ni matarajio yetu kwamba uhamaji huu utakamilika kwa kuzingatia ratiba iliyopangwa kabla ya tarehe 30, Juni 2015.

26.           Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Wizara kwa kushirikiana na TCRA imesajili vituo nane (8) vya redio na vituo viwili (2) vya televisheni na hivyo kuwezesha Tanzania kuwa na jumla ya vituo 93 vya redio na 28 vya televisheni. Aidha uhamaji kutoka mfumo wa utangazaji wa analoji kwenda mfumo wa dijiti umesadia kupanua wigo wa masafa na kuongeza ubora wa matangazo.

27.           Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014, Kamati ya Maudhui ilipokea na kushughulikia malalamiko 7 ya vituo vya televisheni na redio kutokana na kurusha vipindi ambavyo vilikiuka maadili ya utangazaji. Kituo binafsi cha televisheni kilicholalamikiwa kwa kurusha kipindi kilichokiuka kanuni na maadili ya utangazaji kilipewa onyo. Aidha, vituo 6 vya redio vilivyolalamikiwa kwa kurusha vipindi vilivyokiuka kanuni za utangazaji na maadili ya uandishi wa habari vilipewa onyo na vingine kutozwa faini kati ya Shilingi 200,000 na Shilingi 5,000,000.  

28.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, TBC imeendelea kuimarisha upanuzi wa usikivu wa Redio na Televisheni ya Taifa. TBC pia ilirusha matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja. Aidha, TBC ilirusha matangazo ya Bunge Maalum la Katiba kwa lugha za alama kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum. Pamoja na kazi hizo, TBC inakabiliwa na tatizo la uchakavu wa vifaa vya kurushia matangazo. Uchakavu huo wakati mwingine umesababisha tatizo la kukatika kwa matangazo yakiwemo matangazo ya Bunge. 

29.             Mheshimiwa Spika, naomba waheshimiwa wabunge wawe wavumilivu kwani Wizara imejipanga katika kuendelea kutatua changamoto hizo ili kuboresha huduma zitolewazo na TBC. Kupitia Bunge lako Tukufu niwaombe Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono kufanikisha malengo tuliyojiwekea.


30.             Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kutatua changamoto za TBC, mwezi Aprili, 2014 imepokea gari jipya la kisasa la matangazo kutoka Serikali ya Watu wa China. Gari hili litasaidia sana kuongeza nguvu katika kupunguza tatizo la uchakavu wa vifaa. Sambamba na hatua hizo, Wataalamu watano (5) wa TBC walipelekwa nchini China kupata mafunzo maalum ya namna ya kutumia gari hilo pamoja na vifaa husika.

31.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) imeendelea na mkakati wa upanuzi wa kiwanda cha uchapaji. Katika mkakati huo, makubaliano na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) yamekamilika ambapo TIB itaipatia TSN mkopo wa Shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kujenga jengo la kitega uchumi.

32.             Mheshimiwa Spika, katika kupanua wigo wa mapato, TSN na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wameingia mkataba wa ubia wa kuendeleza kiwanja kilichopo Kitalu Na. 27, Central Business Park, Dodoma, kwa ajili ya kujenga jengo la kupangisha. Maandalizi ya ujenzi yameanza.

33.             Mheshimiwa Spika, katika kuboresha magazeti, TSN imeongeza kurasa za habari katika magazeti ya ‘Daily News’ na Habari Leo. Vilevile, imeongeza weledi katika uhariri wa taarifa ndani ya magazeti hayo. Uchapaji wa magazeti hayo unazingatia sera na maadili ya uandishi wa habari.

34.             Mheshimiwa Spika, katika kuboresha usambazaji wa magazeti, Kampuni imepata pikipiki 20 toka Serikali ya Watu wa China kwa ajili ya usambazaji wa mijini. Aidha, TSN, imeingia makubaliano na kampuni za  usafirishaji kusafirisha magazeti ndani na nje ya nchi ili kuwezesha upatikanaji wa habari kwa wakati.

SEKTA YA MAENDELEO YA VIJANA

35.             Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia masuala ya vijana mwaka 2013/2014, Wizara imekabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo, baadhi ya Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya kutokuajiri Maafisa Vijana, uelewa mdogo wa vijana katika kubuni, kutayarisha maandiko ya miradi, kuanzisha na kutekeleza miradi endelevu.

36.             Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni vijana wengi kukosa ujuzi na maarifa ya ujasiriamali na biashara ikiwa ni pamoja na kukosa ujuzi wa matumizi sahihi ya fedha za mikopo wanazopata kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

37.             Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hizi, Wizara imeendelea kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi kwa kuwapa mafunzo na ujuzi katika maeneo ya ujasiriamali, uanzishaji wa miradi endelevu ya uzalishaji mali, uongozi, stadi za maisha na matumizi sahihi ya mikopo. Mafunzo haya yametolewa kwa vijana 668 katika ngazi ya Mikoa na Wilaya katika mwaka wa fedha 2013/2014.

38.             Mheshimiwa Spika, kutokana na kupungua kwa nafasi za ajira katika sekta rasmi ikilinganishwa na idadi ya vijana wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya vijana imeendelea kuhamasisha vijana kuunda makampuni binafsi ya biashara na vikundi vya kuzalisha mali ili waweze kujiajiri. Mpango huu utasaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

39.             Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha na kuongeza mitaji katika miradi na kampuni za vijana zinazoanzishwa, Wizara imeratibu mpango wa kuanzisha Benki ya Vijana na tayari Mshauri Mwelekezi amepatikana. Mshauri huyo anaendelea na upembuzi yakinifu wa uanzishwaji wa Benki hiyo.

40.             Mheshimiwa Spika, kuhusu Mfuko wa Maendelo ya Vijana, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwongozo wa kusimamia Mfuko huu umeandaliwa na kusambazwa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote tangu mwezi Agosti 2013. Kulingana na Mwongozo huu, kila Halmashauri inahitajika kuanzisha SACCOS ya Vijana ambayo itashughulikia utoaji wa mikopo hii. Hadi kufikia Aprili, 2014, Halmashauri 22 kati ya 151 zimeanzisha SACCOS za Vijana.


41.             Mheshimiwa Spika, jumla ya Shilingi bilioni 6.1 zilitengwa kwa ajili ya Mfuko huu. Hadi Aprili, 2014, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi 2,000,000,000. Kati ya fedha hizo zilizokopeshwa ni Shilingi 172,609,000 kwa Miradi ya vikundi vya vijana 25. Hata hivyo, Wizara inaendelea na uchambuzi wa maombi ya vikundi 1,178 yenye thamani ya Shilingi 8,421,906,750 ili kuweza kuvikopesha vikundi vitakavyotimiza vigezo vilivyobainishwa kwenye mwongozo.

42.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza Programu ya “Elimu ya Stadi za Maisha kwa vijana walio nje ya shule”. Katika kipindi hiki, Wizara imeandaa mafunzo kwa waelimishaji 75 wa kitaifa ambao watatoa mafunzo kwa waelimishaji rika kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Kata. Programu hii itawasaidia vijana kujitambua na kufanya maamuzi sahihi yanayohusu maisha yao.

43.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuhamasisha maendeleo ya wananchi, kudumisha umoja, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru. Kwa mwaka 2013, Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa tarehe 5 Mei, 2013 katika kijiji cha Chokocho, Mkoani Kusini Pemba ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Maadhimisho ya kilele cha mbio hizo yalifanyika mkoani Iringa tarehe 14, Oktoba, 2013 na Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kupitia mbio hizo, jumla ya miradi ya maendeleo 1229 yenye thamani ya Sh. 158,587,667,613.40 ilizinduliwa au kuwekewa mawe ya msingi.  Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2014 umefanyika tarehe 2, Mei 2014 Mkoani Kagera; na Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

44.             Mheshimiwa Spika, sambamba na maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wizara iliratibu maadhimisho ya Wiki ya Vijana kitaifa ambayo yalianza tarehe 8 Oktoba na kuhitimishwa tarehe 14 Oktoba, 2013 mkoani Iringa. Lengo la maadhimisho hayo ni kuwakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini na kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu, ujuzi, kuonesha vipaji na ubunifu wa kazi zao, pamoja na kujenga mtandao na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana.

45.             Mheshimiwa Spika,  Maonesho katika Wiki ya Vijana yalishirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na ofisi za mikoa 10, Idara za Serikali 16, Halmashauri za Wilaya 21, Asasi za Kiraia 14, Vikundi vya Vijana Wajasiriamali 53, Vyuo Vikuu vya Elimu 3 na Taasisi za Kibenki 3. Jumla ya watu waliotembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Vijana ilikuwa ni 39,361. Aidha, katika Wiki hiyo, Vijana 300 kutoka makundi mbalimbali ya Vijana walishiriki katika midahalo ambapo pia walipatiwa mafunzo ya aina tofauti yenye lengo la kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali ya maendeleo ya vijana.

46.             Mheshimiwa Spika, washiriki wa Wiki ya Vijana pia walipata fursa ya kupewa huduma ya ushauri nasaha na upimaji wa VVU/UKIMWI kwa hiari kupitia taasisi zinazojihusisha na afya zilizoshiriki katika maadhimisho hayo, kama vile WAMATA, AMREF – ANGAZA, HOSPITALI YA RUFAA IRINGA na JHPIEGO - UHAI CT. Jumla ya Vijana 613 walipima afya zao wakiwemo wanawake 397 na wanaume 216, kati yao vijana 27 sawa na asilimia 4.4 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU. Vijana waliogundulika kuwa na maambukizi walipatiwa huduma ya ushauri wa namna ya kuishi vizuri na kwa matumaini na jinsi ya kuendelea kupata huduma za afya. 

SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI

47.             Mheshimiwa Spika, athari za utandawazi na maendeleo yenye kasi kubwa ya sayansi na teknolojia vimeendelea kuwa ni changamoto kubwa inayokabili Maendeleo ya Utamaduni.  Mmomonyoko wa maadili ulio dhahiri nchini, sio tu miongoni mwa watoto na vijana bali pia hata baadhi ya watu wazima, ni matokeo ya athari hasi za utandawazi na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia yanayoambatana na matumizi mapana ya televisheni na mitandao anuwai ya kijamii. Kwa upande mwingine, upatikanaji kirahisi wa mitambo ya kurudufu kazi za wasanii, hasa wa filamu na muziki, umeendeleza dhuluma ya kipato kwa wasanii wengi huku ukiwaneemesha mapromota na wasambazaji wa bidhaa za filamu na muziki ambao sio wasanii.

Pamoja na changamoto hizi, Wizara kupitia Sekta ya Maendeleo ya Utamaduni imetekeleza kazi zifuatazo katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.

48.             Mheshimwa Spika, katika kuimarisha ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu za tasnia ya utamaduni, Maofisa wawili walipata mafunzo ya namna ya kuainisha namba za misimbo (code numbers) za sekta ya utamaduni ambazo zitatumika kitaifa na kimataifa. Aidha, Wizara ilifanya tafiti za maktabani za lugha za jamii 10 na utafiti wa uwandani katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ili kuhifadhi sarufi, misamiati na istilahi za lugha ya Taifa - Kiswahili.

49.             Mheshimiwa Spika, mintaarafu utafiti wa mila na desturi, Wizara  ilifanya utafiti wa kina kuhusu mila za jando na unyago miongoni mwa jamii za Wamakonde, Wamakua na Wayao. Utafiti huo umewezesha  kukamilisha maandalizi ya  pendekezo la elementi ya urithi usioshikika ambao hatimaye Serikali itaomba urithi huo uingizwe kwenye orodha ya urithi wa utamaduni wa Dunia unaotambuliwa na UNESCO. Elementi hiyo ni ya ngoma ya “Nankachanga” kutoka kijiji cha Namahonga, Wilaya ya Tandahimba, Mkoa wa Mtwara.

50.             Mheshimwa Spika, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika ipasavyo na fursa za ajira zinazotokana na nchi yetu kuteuliwa kuwa Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika hili, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, iliratibu zoezi la kuwapata Watanzania wenye sifa stahiki za kuajirika katika Kamisheni hiyo. Ajira katika Kamisheni zitashindaniwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ni muhimu kwa Tanzania kuwa na wagombea sadifu ili kuhimili vishindo vya kinyang’anyiro hicho.

51.             Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, kazi ya ukusanyaji wa kumbukumbu za mapambano ya kupigania uhuru nchini iliendelea kufanywa kwa kushirikiana na Maofisa Utamaduni wa Mikoa na Wilaya. Kwa kipindi cha mwaka 2013/2014, jumla ya kumbukumbu 63 zimerekodiwa katika kanzi data ya Programu. Programu hii ni muhimu sana katika kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za Ukombozi wa Bara la Afrika. Wizara inaendelea kutafuta ufadhili kufanikisha malengo ya Programu.

52.             Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo ni wadau wakuu ili kujenga uelewa zaidi wa Programu. Aidha, washirika katika Programu hii kutoka Namibia, Afrika Kusini na Msumbiji walikuja nchini kujifunza namna Tanzania inavyotekeleza shughuli za uhifadhi na utunzaji wa kumbukumbu za historia ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.

53.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) liliandaa na kurusha vipindi 52 vya ‘Lugha ya Taifa’ kupitia TBC Taifa, vipindi 52 vya ‘Kumepambazuka’ kupitia Radio One na  vipindi 52 vya ‘Ulimwengu wa Kiswahili’ kupitia Televisheni ya  Taifa-TBC1.  Vilevile, Baraza lilisoma jumla ya miswada 24 ya vitabu vya taaluma na kuvipatia ithibati ya lugha.

54.             Mheshimiwa Spika, Baraza limeratibu na kutoa huduma ya tafsiri kwa Asasi 14 za Serikali, Mashirika ya Umma, pamoja na watu binafsi. Aidha, huduma ya ukalimani ilitolewa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia, mwezi Julai, 2013 na mwezi Januari, 2014.  Vilevile, ukalimani ulifanyika kwenye Mkutano wa Bunge la Afrika nchini Afrika Kusini mwezi Novemba, 2013 na Machi, 2014.

55.             Mheshimiwa Spika, Baraza limeendelea kufuatilia matumizi ya Kiswahili na kubaini jumla ya makosa 75 yaliyofanywa na vyombo vya habari na watumiaji wengine wa Kiswahili kwa kusahihisha na kutoa ushauri wa matumizi stahiki. Baraza katika kujiimarisha, limeongeza wigo wa kiutendaji kwa kuandaa Kamusi Kuu ambapo fafanuzi za maneno (utomeshaji) zimeingizwa na warsha tatu za kuhakiki zimefanyika.

56.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeendesha midahalo 52 ya Jukwaa la Sanaa kwa wasanii, waandishi wa habari na wadau wa sanaa 3,850. Vilevile, Baraza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sanaa, limeendesha mafunzo ya utambaji wa hadithi, ngoma za asili kwa watoto 200 wa shule za msingi katika Mkoa wa Dar es Salaam kati ya Februari na Machi, 2014 kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vyao katika fani husika.

57.             Mheshimiwa Spika, Baraza limeendesha mafunzo  na kuhamasisha watumishi 34 wa Baraza, wasanii na wadau 98 kupitia Jukwaa la Sanaa kuhusu umuhimu wa kujikinga na maambukizi ya VVU na UKIMWI.  Baraza limeendelea kuingiza taarifa muhimu za wasanii na wadau wa sanaa za muziki katika mfumo wa kielektroniki unaounganisha Taasisi za TRA, COSOTA, Bodi ya Filamu na BASATA. Hii itaimarisha urasimishaji wa tasnia ya muziki. Aidha, Baraza limeendelea na hatua za awali za uandaaji wa mfumo wa kanzi data za wasanii mahiri na kukusanya taarifa zao muhimu.

58.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Bodi ya Filamu imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza pamoja na Kanuni zake. Bodi, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea kuhimiza matumizi ya stempu za kodi. Hadi sasa, jumla ya wadau 86 wamechukua Stempu 4,380,000 zilizotolewa kwa upacha (duplicate) kwa ajili ya kuweka kwenye kazi za filamu na muziki. Kati ya hizo 3,810,000 ni kwa kazi za filamu na 570,000 ni za muziki.

59.             Mheshimiwa Spika, Bodi imepitia miswada 139 ya kutengenezea filamu kwa watengenezaji wa ndani na nje ya nchi.  Hadi kufikia Aprili, 2014, jumla ya filamu 1,206 sawa na CD 2,412 zilikaguliwa na kuwekewa madaraja. Kati ya filamu hizo, 127 zilifanyiwa marekebisho. Filamu 7 hazikuruhusiwa kuonyeshwa hadharani. Aidha, kati ya filamu 215 za nje zilizowasilishwa, filamu 2 zilielekezwa kufanyiwa marekebisho. Jumla ya filamu 5 za nje zilizowasilishwa zilizuiliwa kuonyeshwa hadharani. Aidha, Bodi imekagua na kuidhinisha maeneo 13 ya uzalishaji wa filamu.

60.             Mheshimiwa Spika, Bodi imeendelea kutoa elimu kuhusu urasimishaji wa tasnia ya filamu kupitia matangazo kwenye magazeti, vipeperushi, mabango ya barabarani, maadhimisho na sherehe mbalimbali, vipindi mbalimbali vya TV na Redio na vikao vya wadau.

61.              Mheshimiwa Spika, Bodi ilihamasisha wadau kushiriki katika tuzo mbalimbali za filamu kitaifa na kimataifa ambapo hadi kufikia Aprili 2014, jumla ya filamu 10 ziliingia katika tuzo mbalimbali na filamu ya Mdundiko ya Kitanzania ilishinda katika tuzo ya kimataifa huko Marekani.

62.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) iliendesha mafunzo ya stashahada kwa wanachuo wapatao 238 na mafunzo ya muda mfupi kwa wasanii 255 walio kazini. Vilevile, inaendelea na kazi ya kukamilisha mitaala ya shahada ya kwanza ya sanaa za maonyesho na ufundi.

63.             Mheshimiwa Spika, TaSUBa ilisimamia na kuendesha tamasha la 32 la Sanaa na Utamaduni wa Mtanzania ambapo vikundi 40 vya sanaa za maonyesho na vikundi 12 vya sanaa za ufundi vya ndani na nje ya nchi vilishiriki. Aidha, TaSUBa ilishiriki mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyoitishwa kujadili mustakabali wa vituo vya Jumuiya vyenye ubora uliotukuka (Centre of Exellence), ambapo TaSUBa ni kimojawapo cha vituo hivyo.


SEKTA YA MAENDELEO YA MICHEZO

64.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara imeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo uchache wa wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali za michezo, upungufu wa miundombinu inayokidhi mahitaji ya sasa, mwamko mdogo wa jamii kushiriki katika michezo na udhaifu wa uongozi katika baadhi ya vyama mbalimbali vya michezo.

Pamoja na changamoto hizo, Wizara katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014 imetekeleza kazi zifuatazo.

65.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa mafunzo ya Stashahada ya Elimu ya Ufundishaji Michezo na Stashahada ya Uongozi na Utawala kwa wanachuo 40 katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo, Malya, mkoani Mwanza. Aidha, Wizara imeendesha Mafunzo ya muda mfupi ya fani mbalimbali za michezo kwa vijana 200, walimu 100 wa shule za Msingi, walimu 100 wa shule za Sekondari, Viongozi wa Michezo na Makocha 102 katika Vituo vya Michezo vya Kanda ya Kaskazini (Arusha) na Kusini (Songea). Hivi sasa zaidi ya asilimia 50 ya walimu ambao hushiriki katika uendeshaji na ufundishaji wa michezo kwa ajili ya mashindano ya shule za msingi (UMITASHUMTA) na shule za sekondari (UMISETA) ni wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Vituo vya Michezo na Mpango wa Michezo kwa Jamii.

66.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano wa kimataifa na kufuatilia utekelezaji wa Mikataba kati ya nchi marafiki na Tanzania katika Sekta ya Michezo.  Kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Wizara imekamilisha hatua za awali za kujenga miundombinu ya Mchezo wa kupanda Majabali (Rock Climbing) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Wizara iliendesha Kongamano la Kimataifa la Viongozi Wanawake wa Michezo lililofanyika Dar es Salaam tarehe 16 – 18 Desemba, 2013 na kushirikisha jumla ya nchi 17 za Bara la Afrika na Ulaya.

67.             Mheshimiwa Spika, Wizara, kwa kushirikiana na Vyama vya Michezo, imeendelea kufanya maandalizi ya timu za Taifa zitakazoshiriki kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland, mwezi Julai, 2014.  Timu za Michezo ya Riadha, Ngumi, Kuogelea, Mieleka, Baiskeli, Judo, Paralimpiki na Mpira wa Meza zinatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo. Aidha, kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, timu sita za Taifa za mchezo wa Riadha, Ngumi, Kuogelea, Judo, Kunyanyua Vitu vizito na Mpira wa Meza zimepata fursa ya kuweka kambi za mazoezi nchini China, Uturuki, Ethiopia na New Zealand kwa ajili ya maandalizi ya michezo ya Jumuiya ya Madola.

68.             Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia ukamilishaji wa ukarabati wa Uwanja wa Uhuru ambao ni sehemu ya eneo Changamani la Michezo lililoko Dar es Salaam. Ukarabati huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2014.

69.             Mheshimiwa Spika, Wizara ilitoa huduma ya Kinga na Tiba kwa wanamichezo na wadau wa michezo 108,000 wa timu za michezo mbalimbali. Vilevile, Wizara imeendelea na upimaji na utoaji wa elimu kwa wanamichezo kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu haramu za kuongeza nguvu katika michezo.

70.             Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kupambana na dawa na mbinu haramu za kuongeza nguvu michezoni, Wizara imeendelea kutumia matukio ya michezo kama vile Ligi Kuu ya Vodacom, Kambi za Timu za Taifa na Mashindano ya Riadha na Ngumi ya Kitaifa na Kimataifa, kuchukua sampuli mbalimbali (damu, mate, jasho n.k) za wanamichezo kwa ajili ya vipimo vya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu katika michezo kwa uchunguzi zaidi kwenye maabara zilizoko nchini Afrika Kusini. Hadi kufikia Aprili, 2014 wanamichezo 27 walichukuliwa vipimo. Hata hivyo, hakuna aliyegundulika kutumia dawa na mbinu haramu baada ya majibu ya maabara.

71.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa kushirikiana na “UK Sport” na “British Council”, kupitia mradi wa “International Inspiration”, limekamilisha uandaaji wa mifumo rasmi ya Elimu na Ithibati ya Ufundishaji wa Michezo Nchini; Michezo Shirikishi kwa Jamii; Ufuatiliaji na Tathmini ya Maendeleo ya Michezo Nchini; na Utambuzi na Ukuzaji wa Vipaji vya Michezo Miongoni mwa Vijana. Mifumo hiyo inalenga kuinua maendeleo ya michezo nchini na inaendelea kufanyiwa majaribio kwa ajili ya utekelezaji.

72.             Mheshimiwa Spika, Baraza limeendesha mafunzo ya utawala bora kwa vyama vya michezo 17, na kusimamia uchaguzi kwa vyama na mashirikisho ya michezo 14. Aidha, kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Baraza, limeendesha mafunzo ya michezo kwa jamii kwa walimu 76 wa shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Mtwara Vijijini.

73.             Mheshimiwa Spika, Baraza liliandaa na kuendesha Kongamano la Kimataifa kuhusu Mfumo wa Elimu ya Michezo kwa Jamii kwa Nchi za Kanda ya V ya Michezo Barani Afrika. Kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuangalia namna ya kuwa na mfumo mmoja wa utoaji wa Elimu ya Michezo kwa Jamii miongoni mwa nchi wanachama.  Kongamano hilo lilifanyika mwezi Novemba, 2013 huko Arusha na kuhudhuriwa na nchi saba ambazo ni Uganda, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Misri, Zimbabwe na Tanzania.

74.             Mheshimiwa Spika, Baraza limeendesha mafunzo ya uamuzi na ukocha kwa walimu na wanafunzi 761, kati ya hao walimu ni 421 na wanafunzi ni 340. Mafunzo haya, yaliyo katika majaribio ya mradi wa “International Inspiration” yamefanyika katika mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Ruvuma, Mwanza na Mjini Magharibi, Zanzibar.

75.              Mheshimiwa Spika, Baraza, kwa kushirikiana na Asasi ya Kimataifa ya “Tackle Africa” inayojishughulisha na utoaji wa elimu ya kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kutumia mchezo wa soka,  liliendesha mafunzo kwa wanawake 140 na wasichana 8,000 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Lindi.


UTAWALA NA MENEJIMENTI YA RASILIMALI WATU

76.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014, watumishi 51 wamehudhuria mafunzo katika fani mbalimbali.  Kati ya hao, watumishi thelathini na wawili (32), wamehudhuria mafunzo elekezi ambayo yaliandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali.  Aidha, watumishi kumi na saba (17) wamehudhuria mafunzo ya muda mrefu ndani ya nchi na watumishi wawili (2) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi.

77.             Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha Utawala Bora na ushirikishwaji watumishi sehemu za kazi, Wizara imeandaa na kuendesha vikao viwili vya Baraza la Wafanyakazi pamoja na kusimamia uendeshwaji wa vikao mbalimbali vya kiutawala katika kuimarisha utendaji kazi.

78.             Mheshimiwa Spika, katika usimamizi wa haki na maslahi ya watumishi, Wizara imewapandisha vyeo watumishi 32 wanaostahili kwa kuzingatia miundo ya kada zao, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma toleo la mwaka 1999 na 2008 pamoja na taarifa za Upimaji Kazi wa Wazi (OPRAS).

D: MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2014 / 2015

79.             Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2014/2015 umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016; Malengo ya Taifa ya MKUKUTA II; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2010 – 2015; Mpango Mkakati wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo 2011/2012 – 2015/2016; Maagizo ya Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoyatoa kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa nyakati tofauti; Mwongozo wa Utayarishaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2014/2015 na ushauri uliotolewa na Bunge pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kwa nyakati tofauti.

SEKTA YA HABARI

80.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo:-
         (i)   Kuisemea Serikali katika masuala muhimu yanayohitaji ufafanuzi kwa wananchi;
        (ii)  Kukusanya habari mbalimbali za matukio ya kiserikali na kuyasambaza kwa wananchi;
       (iii) Kuratibu Vitengo vya Mawasiliano Serikalini;
        (iv) Kusajili magazeti na machapisho;
         (v)  Kuandaa jarida la Nchi Yetu na kulisambaza;
        (vi) Kuratibu waandishi wa habari katika shughuli za kitaifa na kimataifa na
       (vii)      Kuratibu utekelezaji wa Mradi wa Habari kwa Umma.

81.             Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linakusudia:-

         (i)   Kurusha matangazo ya vikao vya Bunge;
        (ii)  Kulipia huduma ya kukodi “satellite” kwa ajili ya matangazo ya moja kwa moja ya televisheni;
       (iii) Kuhamisha na kujenga mitambo miwili (2) ya FM katika maeneo ya StarMedia (T) Ltd ili kuboresha usikivu wa matangazo ya redio. Maeneo yatakayohusika na zoezi hilo la uhamishaji wa mitambo yake ya FM ni Iringa na Dodoma;
        (iv) Kujenga mtambo mpya mmoja (1) wa FM redio kwa ajili ya kuboresha usikivu wa matangazo katika eneo la Ngorongoro mkoani Arusha na
         (v)  Kujenga studio mbili (2) za redio katika Mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma pamoja na kufunga vifaa vya kisasa.

82.             Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa mwaka 2014/2015 imepanga kutekeleza yafuatayo:-

            (i)      Kukamilisha mradi wa upanuzi wa kiwanda cha uchapaji na
           (ii)       Kuendelea na mchakato wa kuendeleza kiwanja kilichopo Kitalu Na. 27, Central Business Park, Dodoma, kwa ubia na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

83.             Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, Wizara kupitia Kamati ya Maudhui ya Utangazaji imepanga kutekeleza yafuatayo:-

(i)      Kupitia na kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria na Kanuni za Utangazaji;
(ii)    Kutengeneza rasimu ya kanuni ndogo za maudhui ya Utamaduni wa Mtanzania;
(iii)  Kutengeneza  mwongozo wa udhamini wa matangazo (Codes of Advertising and Sponsorship);
(iv)   Kuanzisha utaratibu wa kutoa motisha (Incentive scheme) kwa watengenezaji na vituo vya utangazaji vitakavyorusha vipindi vyenye maudhui bora ya Mtanzania;
(v)     Kuendesha warsha za mashauriano na wadau wa maudhui wa kujitegemea na
(vi)   Kusimamia awamu ya pili ya uhamaji kutoka mfumo wa analoji kwenda mfumo wa dijiti katika miji yote ambayo haijafikiwa na mfumo huu mpya.

SEKTA YA MAENDELEO YA VIJANA

84.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-

(i)      Kuratibu mafunzo ya Ujasiriamali; Uanzishaji na Uendeshaji wa Miradi na Kampuni Endelevu, Uongozi na Stadi za Maisha kwa viongozi wa vikundi vya vijana vya uzalishaji mali na asasi za vijana ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajirika, hivyo kujikimu kiuchumi na kijamii;
(ii)    Kuratibu Mbio za Mwenge wa Uhuru ili kuhamasisha wananchi kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Aidha, Wizara itaratibu maadhimisho ya Wiki ya Vijana ili kuwapa fursa za kubadilishana uzoefu, ujuzi, kuonesha vipaji  na kazi zao za uzalishaji mali, ubunifu pamoja na kuwawezesha kujenga mitandao baina yao na wadau mbalimbali;
(iii)  Kuendelea na maandalizi ya uanzishwaji wa Benki ya Vijana ili kuwezesha vijana pamoja na SACCOS za vijana kupata mitaji kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi;
(iv)   Kuendelea kuwezesha Vijana kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili waweze kujiajiri wenyewe na hivyo kupunguza tatizo la ajira miongoni mwao na umaskini kwa ujumla na
(v)     Kuimarisha vituo vitatu vya mafunzo ya vijana ili viweze kutumika ipasavyo katika kutoa mafunzo ya ujasiri, ujasiriamali, uongozi na stadi za maisha.

SEKTA YA MAENDELEO YA UTAMADUNI

85.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara itatekeleza majukumu yafuatayo:-

(i)      Kuratibu mjadala wa Kitaifa kuhusu maadili ya Mtanzania;
(ii)    Kukuza na kuendeleza matumizi sanifu na fasaha ya lugha ya Kiswahili na kufanya utafiti wa msamiati wa lugha za jamii;
(iii)  Kuratibu mikutano, matamasha ya sanaa na ushiriki wa wasanii katika Sherehe za Kitaifa;
(iv)   Kuratibu utafiti, uhifadhi na uorodheshaji wa urithi wa utamaduni na
(v)     Kuratibu utekelezaji wa miradi ya Ujenzi wa Jumba la Utamaduni na Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika.

86.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-

      (i)      Kuandaa na kurusha vipindi 52 vya ‘Lugha ya Taifa’ katika TBC Taifa, vipindi 52 vya ‘Kumepambazuka’ katika Radio One na vipindi 52 vya ‘Ulimwengu wa Kiswahili’ katika Televisheni ya Taifa (TBC1) ili kuhamasisha na kuelimisha matumizi sahihi ya Lugha ya Kiswahili;
    (ii)      Kusoma Miswada ya vitabu vya taaluma na kuipatia ithibati ya lugha;
  (iii)      Kuratibu na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani katika mikutano ya kitaifa na kimataifa, shughuli za mashirika, makampuni na watu binafsi;
   (iv)      Kuchunguza makosa ya Kiswahili yanayofanywa na vyombo vya habari na watumiaji wengine na kufanya masahihisho ya makosa hayo;
     (v)      Kuandaa Kamusi Kuu ya Kiswahili Sanifu;
   (vi)      Kuchapisha Kitabu cha Furahia Kiswahili (Kiswahili kwa Wageni) na
 (vii)      Kukarabati majengo ya ofisi yaliyonunuliwa kutoka Shirika la Bima la Taifa.

87.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-

         (i)   Kuendesha mafunzo ya utambaji hadithi, ngoma za asili na uigizaji kwa watoto 200 wa shule za msingi 5 za Mkoa wa Dar es salaam kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto katika fani husika;
       (ii)   Kuendesha mafunzo ya sanaa na ujasiriamali kwa wasanii 100 katika mkoa wa Tabora;
     (iii)   Kuendesha midahalo 30 kwa wasanii, waandishi wa habari na wadau wa sanaa 3,000;
      (iv)   Kusajili wasanii na wadau wanaojishughulisha na shughuli za sanaa katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro na Mbeya;
        (v)   Kusanifu, kuboresha na kuhifadhi maelezo ya wasanii katika kanzi data ya BASATA;
      (vi)   Kutoa elimu ya urasimishaji wa tasnia ya muziki kwa wadau wa sanaa na
    (vii)   Kuendelea na ujenzi wa Ukumbi wa Wazi wa sanaa na mafunzo.

88.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, Bodi ya Filamu imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo;

         (i)   Kuendelea na Urasimishaji wa Tasnia ya Filamu;
       (ii)   Kukagua na kuweka madaraja ya filamu 600;
     (iii)   Kupitia miswada 150 ya kutengeneza filamu na kutoa vibali 150 vya kutengeneza filamu kwa waombaji wa ndani na nje ya nchi;
      (iv)   Kuendelea kutoa elimu ya kulinda Maadili ya Mtanzania kupitia tasnia ya filamu na
        (v)   Kufanya utafiti wa masuala ya filamu na kuendesha mafunzo ya kujenga weledi kwa wadau 150 wa filamu.

89.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo:-

      (i)      Kuendesha mafunzo ya stashahada kwa washiriki 250 na mafunzo ya muda mfupi kwa wasanii 270 walio kazini;
    (ii)      Kusimamia na kuendesha Tamasha la 33 la Sanaa na Utamaduni wa Mtanzania na
  (iii)      Kuboresha studio ya picha jongefu na kununua vifaa vya muziki.

SEKTA YA MAENDELEO YA MICHEZO

90.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara itatekeleza yafuatayo:-

      (i)      Kuratibu ushiriki wa timu za Taifa kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland, mwezi Julai 2014;
    (ii)      Kutoa mafunzo ya Stashahada ya Elimu ya Ufundishaji wa Michezo na Stashahada ya Utawala na Uongozi wa Michezo katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya;
  (iii)      Kutoa huduma ya tiba na kinga kwa wanamichezo na kuendelea na juhudi za kudhibiti matumizi ya dawa na mbinu haramu za kuongeza nguvu katika michezo;
      (iv)   Kuendesha mafunzo ya muda mfupi ya fani mbalimbali za michezo kwa wadau 200 katika Vituo vya Michezo vya Kanda ya Kusini (Songea) na Kaskazini (Arusha);
        (v)   Kusajili Vyama na Vilabu vya Michezo;
      (vi)   Kuimarisha uendeshaji wa michezo shuleni na ubora wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA kwa kutoa nafasi zaidi kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kupata mafunzo ya ufundishaji wa michezo mbalimbali katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, Vituo vya Michezo vya Arusha na Songea na fursa nyingine kwa kadri zitakavyopatikana;
    (vii)   Kuratibu ukamilishaji wa Uboreshaji wa Uwanja wa Uhuru na  
  (viii)   Kuratibu uendeshaji wa Uwanja wa Taifa na uboreshaji wa miundombinu katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

91.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Baraza la Michezo la Taifa (BMT) litatekeleza yafuatayo:-

      (i)      Kuandaa na kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa walimu 200 wa michezo kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za serikali za mitaa kupitia Mpango wa Michezo Jumuishi kwa Jamii “Integrated Community Sports”;
    (ii)      Kutoa mafunzo ya Utawala Bora katika Sekta ya Michezo kwa viongozi wa Mashirikisho na Vyama Vya Michezo katika ngazi mbalimbali;
  (iii)      Kuratibu na kusimamia chaguzi za Vyama Vitano (5) vya Michezo na
   (iv)      Kuhamasisha wadau mbalimbali wa Michezo kushiriki katika majaribio ya kutumia mifumo rasmi ya michezo katika kutekeleza Programu zao za Maendeleo ya Michezo nchini.

UTAWALA NA MENEJIMENTI YA RASILIMALI WATU

92.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo:-

      (i)      Kuendelea kuwajengea uwezo watumishi kwa kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa kuzingatia makundi ya kada zao.  Mafunzo hayo yatalenga katika kuimarisha utendaji kazi. Aidha, Wizara itatoa elimu ya maadili kwa watumishi ili kuimarisha nidhamu ya kazi;
    (ii)      Kuendelea kuhamasisha watumishi kukubali kupimwa UKIMWI ili kutambua hali zao.  Aidha, Wizara itaendelea kutoa msaada wa chakula na lishe kwa watumishi wanaoishi na VVU na UKIMWI ambao wamejitokeza;
  (iii)      Kuhakikisha watumishi wanaostahili wanapandishwa vyeo kwa kuzingatia miundo ya kada zao, Sera ya Menejimenti katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1999 na 2008 pamoja na taarifa za Upimaji Kazi wa Wazi (OPRAS) na
   (iv)      Kuendelea kuimarisha utawala bora na ushirikishwaji watumishi sehemu za kazi kwa kuendesha vikao vya Baraza la Wafanyakazi pamoja na vikao vingine vya kiutawala ili kuimarisha utendaji kazi.

E: HITIMISHO

93.             Mheshimiwa Spika, Wizara itaendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Sekta inazozisimamia ili ziweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya nchi yetu. Hii ni pamoja na kuongeza ajira, kipato, kulinda mazingira, kudumisha amani na mshikamano katika jamii. Wizara itaendelea kukabiliana na changamoto zilizoainishwa katika hotuba hii ili zipatiwe ufumbuzi ili fursa zinazopatikana katika Sekta za Wizara ziweze kutumika ipasavyo katika kuleta maendeleo ya nchi. Napenda kuwahakikishia wananchi ya kwamba Wizara ina nia thabiti ya kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo hatua kwa hatua kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.


SHUKRANI

94.             Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukrani za dhati kwa wote walioshirikiana nasi katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 katika kutimiza malengo yetu. Ushirikiano huu utaendelezwa na kuimarishwa zaidi kwa manufaa ya Taifa ili kuhakikisha kuwa  umma wa Watanzania unapata taarifa za kina  na za uhakika, vijana wanaendelea kujiajiri na kuajirika, maadili na utamaduni wa Mtanzania unazingatiwa, pamoja  na kuwa Taifa lenye ufanisi kupitia michezo. Mafanikio ya utekelezaji wa majukumu na malengo ya Wizara yamewezekana kutokana na ushirikiano uliopo miongoni mwa viongozi na watumishi wa Wizara na wadau wengine walio nje ya Wizara.

95.             Mheshimiwa Spika, shukrani zangu za pekee ziende kwa  Mhe. Alhaji Juma Suleiman Nkamia (Mb.), Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye amekuwa msaada mkubwa kwangu, Bibi Sihaba  Nkinga, Katibu Mkuu na Prof. Elisante Ole Gabriel, Naibu Katibu Mkuu. Ninawashukuru kwa uchapakazi wao mahiri na ushirikiano mkubwa walionipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, nawashukuru Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo, Watendaji Wakuu wa Asasi, Wataalamu na Watumishi wote wa Wizara kwa juhudi walizofanya kuhakikisha kwamba tunatimiza ipasavyo majukumu tuliyokabidhiwa na Taifa.

96.             Mheshimiwa Spika, napenda niwashukuru Wenyeviti na wajumbe wa Bodi za Asasi zilizo chini ya Wizara kwa jinsi wanavyofanya kazi kwa kushirikiana na Wizara. Asasi hizo zimefanya kazi kwa karibu sana na mimi na nawaomba waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa ili kuhakikisha Wizara yetu inafikia malengo yake.

97.             Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa nitumie fursa hii tena kuwashukuru washirika wetu wa maendeleo ambao wametuunga mkono wakati wote wa kutekeleza majukumu ya Wizara.  Shukrani hizi ziwaendee wahisani waliotusaidia, nikitarajia kuwa wataendelea na moyo huo. Siyo rahisi kuwataja wote lakini nitaje wachache ambao ni Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Finland, Uingereza, Denmark, Japan, Sweden, Norway, Iran, Cuba, Ethiopia, New Zealand, Turkey, Korea ya Kusini, Marekani na Ujerumani pamoja na Mashirika ya Kimataifa ya UNESCO, UNICEF, UNFPA, IYF, UNDP, ILO, Forum - SYD, BRAC, Balton Tanzania Limited, JICA, CYP, ESAMI, RALEIGH INTERNATIONAL, VSO, AMREF, Restless Development na BRITISH COUNCIL.

98.             Mheshimiwa Spika, napenda kuvishukuru vyombo vyote vya habari nchini ambavyo vimefanya kazi nzuri ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha umma. Ninaamini kuwa vyombo hivyo vitaendelea na kazi hiyo kwa kuzingatia maadili na weledi. Aidha, ninamshukuru sana Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii kwa wakati, bila kuvisahau vituo vya Televisheni na Redio ambavyo kwa namna ya pekee vinarusha hotuba hii hewani moja kwa moja.

MAKADIRIO YA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

Mapato

99.             Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara imepanga kukusanya jumla ya Shilingi 1,149,008,000 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya mapato. Mchanganuo wa makusanyo kifungu kwa kifungu kwa mwaka 2013/2014 na Makadirio kwa mwaka 2014/2015 upo katika Kiambatisho Na. I.

Matumizi ya Kawaida

100.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara imetengewa jumla ya Shilingi 20,371,844,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (Matumizi Mengineyo na Mishahara), fedha hizo zinajumuisha:-
(i)   Mishahara ya Wizara Sh.  3,151,654,000
(ii)            Mishahara ya Asasi   Sh.  7,849,270,000
(iii)  Matumizi Mengineyo
ya  Wizara -            Sh. 5,830,920,000.
(iv)   Matumizi Mengineyo
 ya  Asasi                     Sh. 3,540,000,000.

Mchanganuo wa makadirio ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara na Asasi upo katika Kiambatisho  Na. II. Matumizi ya Kawaida kwa Wizara peke yake rejea Kiambatisho Na. III na kwa Asasi rejea Kiambatisho Na. IV.

Miradi ya Maendeleo

101.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara imetengewa jumla ya Shilingi 15,000,000,000 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Mchanganuo kamili upo katika Kiambatisho  Na.  V.

MAOMBI YA FEDHA KWA AJILI YA KUTEKELEZA MPANGO WA MWAKA 2014/2015.

102.         Mheshimiwa Spika, ili Wizara iweze kutekeleza majukumu na malengo yake ya mwaka wa fedha 2014/2015, naomba sasa Bunge  lako  Tukufu  liidhinishe  bajeti  ya jumla ya Shilingi 35,371,844,000 ambapo kati ya  hizo,  fedha za Matumizi ya Kawaida ni Shilingi 20,371,844,000 na Fedha za Miradi ya Maendeleo ni Shilingi 15,000,000,000.  Mchanganuo wa fedha hizi upo katika viambatisho vilivyotajwa hapo awali ambavyo ni sehemu ya Hotuba hii.

103.         Mheshimiwa Spika, napenda nitoe tena shukrani zangu za dhati kwako binafsi na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza. Hotuba hii inapatikana pia katika tovuti ya Wizara kwa anuani ya: www.habari.go.tz na www. tanzaniangovernment.blogspot.com

104.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: