ZAIDI YA VYAMA 10 VYA UPINZANI BADO VIMO BUNGE LA KATIBA

Zaidi ya vyama 10 vya siasa vya upinzani visivyo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vyenye wajumbe katika Bunge Maalum la Katiba wamegoma kuunga mkono Ukawa baada ya kuamua kubaki ndani ya Bunge hilo kuendelea na mjadala wa Rasimu ya Katiba.
Ukawa wakiongozwa na mmoja wa viongozi wake, Profesa Ibrahimu Lipumba, juzi walitoka bungeni kwa madai kuwa, mjadala unaoendelea umekuwa wa matusi, ubaguzi na vitisho huku wajumbe wakilazimishwa kuridhia serikali mbili zisizo mapendekezo ya rasimu.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, jana alieleza kupata ujumbe wa uwepo wa wajumbe kutoka katika vyama hivyo na kuwatangazia wajumbe baada ya ombi kutolewa kwamba wajumbe walitaka kufahamu kama bungeni humo, wapo wanasiasa wa vyama vya upinzani.
Akithibitisha uwepo wa wajumbe wa vyama hivyo baada ya kukaribishwa kuthibitisha hilo na Sitta, Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha APPT-Maendeleo, Peter Mziray alivitaja vyama hivyo kwa majina na wajumbe waliokuwemo bungeni walisimama.
“Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kupata fursa hii kwamba mtambue tupo, kwanza niseme tu kwamba tutahakikisha Katiba inapatikana na nimepokea ujumbe wananchi wanawataka warudi, mambo yote yanamalizwa mezani,” alisema Mziray.
Miongoni mwa vyama vilivyotajwa kuwepo bungeni ni pamoja na Demokrasia Makini, ADC, Jahazi Asilia, Wakulima AFP, Tadea, UPDP, TLP, CCK, Chausta, Sauti ya Umma (SAU), UND na chama cha DP kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila ambacho mjumbe mmoja alikuwepo.
Mziray alisema vyama vyao vina usajili wa kudumu na havitaondoka bungeni mpaka Katiba ipatikane kwa mujibu wa sheria. Naye kiongozi wa UDP, Gidion Cheyo alisema wapo bungeni kujadili mustakabali wa nchi ndio maana pamoja na kwamba wengine wao ni Ukawa, hawakutoka bungeni.

No comments: