VIGOGO WALIOHODHI MASHAMBA KUFUTIWA HATIMILIKI

Serikali imeanza mchakato wa kisheria, kumwezesha Rais kufuta hati miliki za ardhi ambayo haijaendelezwa kwa muda mrefu, yakiwemo mashamba ya vigogo yanayodaiwa kugeuzwa vitega uchumi kwa kukodisha wananchi kwa fedha nyingi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene, alisema hayo  jana , mjini hapa katika hotuba yake ya ufunguzi wa warsha ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wakulima Wadogo nchini, ambayo hufanyika Aprili 17 kila mwaka.
Katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania ( Mviwata), Simbachawene alisema Serikali haitakubali kuona watu wachache wakiwemo vigogo, wakimiliki mamia ya hekta za ardhi bila kuziendeleza.
Alisema wizara inaangalia utaratibu wa Serikali  kutwaa  mashamba hayo kwa ajili ya kugawia wakulima wadogo na wananchi wengine watakaoendeleza ardhi husika kwa kilimo.
Simbachawene alisema mbali na mikoa mingine, Morogoro unaongoza kwa uwepo wa watu wachache, wanaohodhi ardhi ya mashamba makubwa ambayo hayaendelezwi na mengine ni mapori.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, baadhi ya wamiliki wa  mashamba  hayo makubwa katika mikoa mbalimbali,  wamegeuza mtaji kwa kukodisha wananchi wanyonge, wasiokuwa na ardhi na  kuwatoza kati ya  Sh 100, 000 na zaidi kwa ekari.
“ Ni mfumo wa kisheria unafanyika ili kuwapokonya ardhi wale vigogo waliohodhi. Si muda mrefu zoezi hili litaanza kufanyika “ alisema.
Alisisitiza, “ Tunawashauri  waachie wenyewe sehemu ya ardhi kwa kuwapatia wananchi, tusianze kurudisha  ‘unyarubanja’...hatutaki kurudi huko  na kama hawataki kujisalimisha, tunayatwaa kwa kuwafutia hati za umiliki wao.”

No comments: