WASIO KATIKA MFUMO RASMI WAKARIBISHWA KUJIUNGA NHIF

Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF) umetaka watu wasio katika mfumo rasmi wa ajira wanaotaka kupewa huduma na mfuko huo kujiunga katika makundi na kuomba kujiunga katika mfumo wa upewaji huduma na mfuko huo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NHIF, Hamis Mdee alisema hayo juzi katika mazungumzo yake na uongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) wakati alipotembelea ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.
"Najua suala la afya ni muhimu na lina changamoto zake nyingi …tulikuwa tukishughulika na watu walio katika mfumo rasmi wa ajira tu, lakini kwa kuwa kwa sasa tunawachukua pia hata wale walio katika mfumo usio rasmi, ni kwa nini wasitumie," alisema Mdee.
Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN, Gabriel Nderumaki alisema kampuni hiyo ipo tayari kusaidiana na mfuko kuhamasisha wananchi kutumia huduma za afya za mfuko huo.
"Sisi kama kampuni kubwa ya magazeti kupitia magazeti yetu yanayofika kila kona ya Tanzania tunaweza kuwafikia Watanzania wengi katika kila wilaya na kuwaeleza namna wanavyoweza kunufaika na huduma hii ya afya," alisema Nderumaki.

No comments: