MABADILIKO MATUMIZI YA BARABARA ZA KATIKATI YA DAR

Katika juhudi za kuimarisha hali ya usafiri na kupunguza msongamano, alama mpya za barabarani na mabadiliko ya njia yanategemewa kufanyika katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwisho wa mwezi huu.
Kuanzia Aprili 28 mwaka huu, uongozi wa Jiji  utaanza kuondoa alama za zamani na kuweka mpya katika maeneo mbalimbali ya katikati.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa alisema jana jijini hapa kwamba mabadiliko hayo yanaendana na matakwa ya utaratibu mpya wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.
“Patakuwa na mabadiliko ya njia na alama mpya ambavyo vitapaswa kufuatwa na kuheshimiwa na madereva wote wa magari na vifaa vingine vya moto,” aliwaambia waandishi wa habari jana.
Silaa alisema mbali na kuhakikisha utaratibu wa mabasi yaendayo haraka unatekelezeka ipasavyo na kwa ufanisi, mabadiliko hayo pia yanalenga kupunguza msongamano katikati ya Jiji.
Pia mabadiliko yanalenga kuongeza ufanisi wa ufanyaji kazi wa mabasi ya daladala na kutoa nafasi kwa baadhi ya eneo la barabara ya Morogoro kubakia kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka na waenda kwa miguu tu.
Akielezea zaidi mabadiliko hayo, mwakilishi wa Halmashauri ya Ilala Kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Tigahwa Serapion alisema mabasi yote yanayopita barabara ya Kilwa yataishia Stesheni na kurudi kupitia njia hiyo.
Yanayopita Barabara ya Nyerere na Uhuru yataishia kituo cha Mnazi Mmoja na kurudi kupitia njia zao.
Pia kutakuwa na mabasi yatakayoanzia Mnazi Mmoja kupitia njia ya Bibi Titi, Maktaba hadi kituo cha Posta ya Zamani Benki ya NBC na kurudi kupitia njia hiyohiyo. 
Serapion alisema mabasi yote yanayopita barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwenda  katikati ya jiji yataishia katika kituo cha YMCA barabara ya Upanga na kurudi kupitia njia hiyo.
Pia barabara ya Sokoine zitaruhusiwa gari binafsi kupita kuanzia Kituo Kikuu cha Polisi kwenda  Kivukoni, Hospitali ya Ocean Road hadi kwenda kuungana na barabara nyingine ikiwemo ya Ali Hassani Mwinyi.
Kwa upande wa barabara ya Samora, badala ya kwenda hadi Hospitali ya Ocean Road sasa magari madogo binafsi yataanzia katika hospitali hiyo kwenda Mnara wa Saa. 
Njia zote za mabasi hayo ya daladala hazitakatiza katika barabara ya mradi wa BRT isipokuwa yanayotoka Mnazi Mmoja kwenda Posta ya Zamani.
Alisema alama zitawekwa kuonesha njia hizo zitakavyokuwa na namna mabasi yanayotoka Mnazi Mmoja yatakavyoweza kukatiza katika barabara ya mradi huo wa mabasi.

No comments: