WAWILI WAOKOTWA WAKIWA WAFU BAADA YA MVUA

Miili ya watu wawili imeokotwa katika sehemu tofauti za Jiji la Dar es Salaam baada ya kusombwa na  mvua kubwa iliyonyesha.
Katika tukio la kwanza, maiti ya Omary Benjamin (15) aliokotwa akielea ndani ya mashimo ya mchanga yaliyojaa maji, maeneo ya Mbande Wilaya ya Temeke.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema  mwili huo ulibainika juzi saa 5 asubuhi.  Alisema mtoto huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili  na alitoweka nyumbani bila ya kuaga, hakuonekana hadi maiti alipokutwa maeneo hayo.
Wakati huohuo,  mtoto mwingine,  Omary Abass (14), mwanafunzi wa kidato cha kwanza, katika Shule ya Sekondari Kitonga, mwili ulikutwa ukielea kwenye mto Mzinga, Yombo Kilakala.
Kwa mujibu wa Kamanda, mwanafunzi huyo alikuwa akijaribu kuvuka mto huo kwa kuogelea juzi.

No comments: