MATUNDA, VYAKULA VYAPUNGUA KWENYE MASOKO DAR

Mvua zilizonyesha mfululizo zimesababisha upungufu wa mazao ya vyakula na matunda katika masoko mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Hayo yalielezwa na na Mkurugenzi wa Soko Kuu la Kariakoo,  Florens Seiya.
Mkurugenzi huyo alisema shughuli za uingizwaji wa mazao sokoni hapo zilisimama kutokana na mvua hizo.
Alisema magari mengi yalikwama nje ya Jiji la Dar es Salaam hali iliyosababisha kukabiliwa na upungufu wa baadhi ya mazao sokoni hapo.
“Kwa kweli mvua  ilileta tabu kidogo kwa sababu shughuli zilisimama kama ilivyo kwingine, mazao yalipungua sana kuna vitu kama nyanya, vitunguu na hoho ziliadimika. Mchele kidogo ilikuwa nafuu kutokana mchele ulikuwepo stoo kwa hiyo walitumia huo,” alisema Seiya.
Aidha, mfanyabiashara na dalali katika Soko la Tandale, Mwinyi Maneno alisema kabla ya juzi meza za wafanyabiashara zilikuwa wazi kutokana na magari kushindwa kufika sokoni hapo.
Katika soko la Mabibo, hali ilikuwa tofauti kwani katika soko hilo baadhi ya magari yalikuwepo hivyo haikuwaathiri sana.
 “Kama ingeendelea ndiyo ingetupa shida lakini kwa siku mbili hizi athari siyo kubwa sana maana kuna magari yalikuwepo,” alisema mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la fadhili Ng’amba.

No comments: