WAJUMBE UKAWA WASHIRIKI MKUTANO WA HADHARA ZANZIBAR

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliotoka bungeni juzi jioni wamepanga kufanya mkutano wa hadhara Zanzibar kesho, kwa kile walichodai ni kuwaeleza wananchi ukweli wa mambo yanayojiri katika Bunge linaloendelea hivi sasa.
Ukawa wameamua kuchukua hatua hiyo, huku Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta akisema ofisi yake ipo tayari kwa mazungumzo na wajumbe hao ikiwa ni njia ya kuwezesha mchakato wa kutunga Katiba kuendelea kwa pamoja na kwa amani.
“Mimi nadhani sababu za kitendo chao walichokifanya jana (juzi) hazitoshi, mlango wangu uko wazi, nimeongea na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na yeye kama kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mlango wake upo wazi kwa mazungumzo,” alisema Sitta jana.
Akizungumza  na wajumbe wa Ukawa kwenye ukumbi wa African Dream  mjini hapa jana, Mjumbe wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuwaeleza ukweli wananchi juu ya mambo yanayoendelea hivi sasa Dodoma.
“Tulitoka jana bungeni kwa sababu hatukuona haja ya kuendelea kuwepo huku lugha zinazotumika ni za matusi, ubaguzi, kejeli  na pia Rasimu iliyokuwa ikijadiliwa sio ile ya Tume iliyowasilishwa bungeni,” alisema Lipumba.
Kutokana na hali hiyo, alisema wameamua kwenda Zanzibar kufanya  mkutano na wananchi na kuwaeleza hayo ikiwa ni pamoja na kuwaeleza kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliyoitoa hivi karibuni wakati alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe za kusimikwa kwa Askofu Joseph wa Kanisa la Methodist mjini hapa.
Alisema wajumbe wote wa Ukawa wasio na dharura watasafiri Jumamosi asubuhi kwenda Zanzibar kushiriki mkutano huo na nia yao ni kutaka Bunge lijadili rasimu ya Katiba mpya iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na sio rasimu ambayo haijawasilishwa na Tume.
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum ilikutana jana ambapo yeye alipewa taarifa kuwa ni Kamati ya Uongozi kuhusu Bunge la Bajeti, lakini alipofika ndani alikuta mjadala unaoendelea ni kuhusu Bunge Maalum, aliondoka.
Wakati Lipumba akijiandaa kwenda kuzungumzia kauli ya Lukuvi, Waziri huyo wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge, jana alirudia kauli hiyo na kusisitiza haina ubaya.
Lukuvi alisema si makosa raia wa Tanzania kuhofia majeshi ya ulinzi kuchukua nchi ikiwa muundo wa Muungano wa serikali mbili ukibadilishwa na kuwa serikali tatu.
Aidha, amesema pia ana hofu kuhusu mwenendo wa   CUF unaoshirikiana kisiasa na Taasisi ya kidini ya Uamsho, inayotekeleza majukumu yake Zanzibar kwamba umelenga kuua Muungano na kuhatarisha amani kwa mgongo wa dini ya Kiislamu.
Lukuvi alisema hayo, alipotoa ufafanuzi wa kauli zake alizozitoa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma wakati wa Ibada ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu wa Kanisa hilo.
Kauli hiyo ndio iliyodaiwa na  Ukawa kuwa moja ya sababu ya kutoka nje ya Bunge kususia kikao. Madai mengine ya Ukawa yalikuwa ni ubaguzi, matusi na vitisho vinavyoendelea bungeni.
Katika ufafanuzi wake Lukuvi alisema kwamba mfumo wa serikali tatu unaweza ukasababisha nchi kupinduliwa na Jeshi  na  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaweza ikaongozwa na  CUF kwa Sera za Kikundi cha Uamsho jambo linalompa hofu ya udini na kuvunjika kwa amani.
Lukuvi ambaye jana alilazimika kukatisha safari yake ya kwenda India kwa matibabu, alisema alichoeleza katika hafla hiyo ya kumsimika Askofu ni hofu zake binafsi kuhusu muundo wa serikali tatu.
“Wote nikiwauliza hapa uamsho ni nani mtasema ni CUF, kwa nini sasa nisiwe na hofu ya kidini wakati kuna chama cha siasa ambacho kinamiliki taasisi inaitwa Uamsho lakini ina ladha ya kidini, hizo ndizo sera zao, unakuwaje na chama cha siasa kinachojipanga kutawala Zanzibar lakini kinaendeshwa na sera za Uamsho?
“Wanachosema CUF ndicho wanachosema Uamsho, wakisema serikali tatu ngangari, wakisema serikali ya mkataba sawa kabisa, wapi umeona vikundi kama hivyo, ukiona chama kinajitayarisha kuchukua madaraka na kinatumia taasisi hii kueneza sera zake ni hatari kwa mustakabali wa nchi,” alisema.
 Akizungumzia hofu ya nchi kupinduliwa, Lukuvi alisema  katika muundo wa Serikali tatu, Rais wa shirikisho hawezi kuwa Amiri Jeshi Mkuu, kutokana na kutokuwa na vyanzo vya mapato hivyo haiwezi kuendesha vyombo vya dola kama Jeshi na Polisi ambao mara nyingi bajeti zao ni kubwa na hazijawahi kutosha hata katika serikali mbili za sasa.
“Kwa mfumo huu wa serikali tatu, tusiwatafutie sababu wanajeshi wetu, mimi nilishasema sitashiriki kutafuta vyanzo kwa serikali ya tatu badala yake naukataa muundo huu,” alisema Lukuvi na kuongeza kuwa katika ukosefu mkubwa wa mapato, majeshi yahawezi kuvumilia lazima kutokee uasi na hiyo ndio hofu yake.

No comments: