ASKOFU AHOJI BUNGENI UKAWA KUGOMBANA NA MAREHEMU

Rais Jakaya Kikwete amewataka wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, kuacha kuwakashifu waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume.  
Amesema yeye hatishwi na vijembe, wanavyotoa baadhi ya wabunge wa Bunge hilo.
Lakini, ameonya waache kutoa vijembe vikali, alivyoviita “vya chini ya mkanda”, mfano kukashifu waasisi wa Taifa.
Rais amesisitiza kuwa ana matumaini makubwa na mchakato wa Katiba mpya, unaoendelea na kwamba anafurahia jinsi mijadala, inavyoendeshwa bungeni.
“Mimi na-enjoy(furahia) sana debate (mjadala). Nataka waendelee kuzungumza kwa uhuru. Mtu akipata nafasi ya kusema, joto linapungua ” alisema Rais Kikwete,  Ikulu, Dar es Salaam juzi,  kwenye mahojiano maalum na TBC1, yaliyohudhuriwa pia na waandishi wa vyombo vingine.
Akifafanua kuhusu vijembe, alisema unaweza kukuta mjumbe anasema “Kikwete nchi imemshinda” au “CCM imeshindwa kutawala.”
Alisema vijembe kama hivyo, havimpi taabu, kwa sababu hayo ni mawazo binafsi ya mjumbe, wakati kwa hali halisi  yeye nchi haijamshinda wala CCM haijashindwa kuongoza. “Lakini vijembe vingine vinapigwa chini ya mkanda, hivi siyo vizuri,” alisema Rais.
Rais alisema wanaotumia lugha chafu (wanaopiga chini ya mkanda), wanakosa adabu na dunia ndiyo itawafundisha.
“Si vizuri kuwashambulia waasisi wa Taifa kwa sababu wamefanya kazi kubwa. Kwa mfano Mzee Karume ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar, yaliyowezesha Waafrika wa Zanzibar kujikomboa kutoka kwa utawala wa Sultan na Waarabu. Mwalimu Nyerere ametuachia Taifa moja, lenye amani na utulivu, lenye makabila 120,” alisema.
Rais alisema Mwenyekiti wa Bunge, Samwel Sitta amemhakikishia kuwa atampa kila mjumbe wa Bunge la Katiba,  nafasi ya kuchangia mijadala  na wale wasiosema, alisema atawaamsha waseme, ili wasije wakatoka na kudai hawakupewa nafasi.
“Mambo yanakwenda vizuri na hili ni jambo jema,” alisema Rais katika mahojiano hayo, ambayo yalichukua muda wa saa mbili.
Aliongeza;“Kuna baadhi ya wajumbe wamekuwa wakinitumia meseji, juu ya lugha kali wanazotumia baadhi ya wabunge, na kuhoji huyu jamaa vipi,  lakini mimi huwajibu kuwa hayo ni mawazo ya mtu binafsi, hiyo ni hulka ya mtu, muacheni aseme alivyofikiria yeye.”
Rais alisisitiza kinachosubiriwa na Watanzania wengi ni wabunge hao, kutengeneza Katiba itakayokubaliwa na wananchi wengi.
Alitoa rai kwa wajumbe hao, wasome vizuri Rasimu ya Katiba mpya sura kwa sura, mstari kwa mstari na neno kwa neno, kuona dhana itakayofaa kwa jamii. 
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, uliopangwa kufanyika mwaka huu, alisema mwaka huu una mwingiliano na mchakato wa Katiba mpya, hivyo wataangalia suala hilo serikalini. 
Mathalani, alisema baada ya Bunge Maalumu la Katiba kukamilisha kazi yake, kutakuwa na muda mwingine wa kura ya maoni, jambo litakaloathiri maandalizi ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa.
Kwa upande wa vyombo vya habari, Rais alisema Serikali imetoa uhuru mkubwa kwa vyombo vya habari nchini; na hakuna wakati wowote tangu Uhuru, ambapo nchi iliwahi kuwa na magazeti mengi, kama wakati huu.
Hata hivyo, Rais alionya kuwa uhuru huo, usiwe wa kuchochea, kubomoa nchi au kuingiza nchi kwenye machafuko.
Alisema Serikali ndiyo yenye dhamana ya kulinda amani na usalama wa nchi, hivyo itachukua hatua kwa chombo chochote cha habari, kitakachofanya uchochezi, kubomoa nchi au kujaribu kutumbukiza nchi kwenye vurugu.
Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemela (pichani juu katikati) ameonya na kulaani kitendo cha wajumbe wa  Ukawa  kuwafananisha wajumbe wengine wa Bunge hilo na wauaji wa kundi la waasi la Intarahamwe lililoongoza mauaji ya kimbari nchini Rwanda.
Askofu Mtetemela pia alisema ukiona mtu anagombana na kumkosoa marehemu (waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume), anasababisha watu wajiulize maswali mengi kwa kuwa marehemu hana nguvu na mwenye uwezo wa kukosoa ubaya wa marehemu ni Mungu mwenyewe.
Mtetemela aliyasema hayo jana, bungeni alipokaribishwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kusema neno kuhusu hali inayoendelea katika mjadala huo baada ya Ukawa kususia Bunge na kutoka nje juzi.
“Ukiona mtu anagombana na marehemu, utajiuliza maswali mengi sana, unakashifu marehemu, asiye na nguvu ya kukujibu, ubaya wa marehemu mwenye uwezo kuukosoa ni Mungu mwenyewe, wewe ni nani, na una kipimo cha kiasi gani kukashifu kiongozi anayesifiwa duniani kote,” alisema Askofu huyo.
Akizungumza kwa masikitiko, Askofu Mtetemela ambaye ni mjumbe kupitia taasisi za dini kundi la 201, alisema, “Profesa Ibrahimu Lipumba, katika mchango wake jana (juzi) alilinganisha Bunge hili na
Intarahamwe wa Rwanda, ni kauli nzito sana kwa mtu maarufu kama Lipumba kuchafua Bunge hili.”
“Intarahamwe ni wauaji, wajumbe wa Bunge hili hawawezi kulinganishwa na hao wauaji, kutuita sisi wauaji ni mbaya, inafufua maumivu ya ndugu zetu wa Rwanda ambao ni juzi tu walikumbuka mauaji yale mabaya ya kimbari, hakuna mtu anayetaka kuua mtu hapa,” alisema Askofu Mtetemela.
“Kwanini tutumie jambo la utata lililotokea kwa wenzetu, wakati tukiwa na tofauti fulani baina yetu na Rwanda? Hili linahitaji kukemewa, tena kwa kuwa limefanywa na kiongozi (Lipumba), angekuwa mtu mwingine tungesema haelewi,” alisema Askofu Mtetemela.
Juzi jioni baada ya wajumbe wengi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge, Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mwigulu Nchemba   alitoa maelezo marefu jinsi Ukawa walivyopanga kukwamisha mchakato huo.
Alisema amefikia hatua ya kuomba muongozo huo kwa sababu jambo hilo halijatokea lakini kwa bahati mbaya ni jambo lililopangwa na halijapangwa juzi peke yake na kutimizwa jana, bali limepangwa tangu kuanza kwa mchakato wa Katiba.
Alisema Watanzania watakumbuka kwamba Bunge  lilipokuwa likitunga Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya Katiba, Ukawa bila kutoa  maoni yao hapo bungeni walitoka nje na kutoa vitisho vingi vilivyowapa hofu wananchi.
Hata hivyo alisema Rais Kikwete kwa unyenyekevu licha ya nguvu kubwa aliyonayo, aliwasihi akutane nao ili kuondoa sintofahamu hiyo, jambo ambalo walilitimiza na kwenda na madai ambayo yangeweza kumalizwa bungeni.
“Bunge likamaliza hatua ya kwanza, hatua ya pili wakaja na madai yaliyowekwa kwenye utaratibu kwa sababu waliyadai, wakayapinga tena na kutoa vitisho pale viwanja vya Jangwani,” alisema Mwigulu.
Aliongeza baada ya vitisho hivyo Ukawa wakasema watatafuta helikopta zaidi ya tano na watazunguka nazo nchi nzima kuhamasisha kutokuwepo  utii wa sheria.
”Watanzania  mtakumbuka jinsi Rais alivyohutubia Taifa kwa unyenyekevu mkubwa akiwaomba wasiende kwenye hatua hiyo, bali wakutane naye watafute suluhu,” alisema Mwigulu.
Hata hivyo upande huo haukuishia hapo, Mwigulu alisema Bunge lilipokuja kutunga kanuni za kuwaongoza wajumbe kwenye Bunge hilo, ripoti kinzani ilizua mambo na kusababisha mabishano ambapo upande wa walio wengi wakapata taarifa kuwa Ukawa wamepanga ikiwa hawatapewa taarifa kinzani, wataharibu mchakato wa Katiba.
Hivyo ripoti kinzani ikatolewa kwa Ukawa na walipokwenda  kwenye ufafanuzi kuhusu ripoti ya wajumbe wote, wajumbe wakasema kutakuwa na saa moja, lakini dakika 20 zitakuwa za wachache, wao wakasema wapewe dakika 30 za ufafanuzi, na kama hawatapewa watatoka nje na mchakato utaishia hapo.
“Wakapewa lakini tulio wengi tukasema maadamu  dakika 20,  ukijumlisha na 30 ni 50 basi walio wengi wana dakika 40 na wapewe nyingine 10 za ufafanuzi, walio wachache wakasema walio wengi wakipewa hizo dakika watajitoa kwenye mchakato na utaishia hapo,“ alisema Mwigulu.
Aliongeza kuwa jambo hilo lilisababisha madai hayo kuishia hapo, kitendo ambacho kiliwashangaza wananchi wengi, kwani  walio wengi hawakupata hata dakika tano kuchambua mawazo yao, ambapo Mwigulu alisema kwa kuwa walio wengi walitaka mchakato uendelee, wakaamua hivyo.
Alifafanua walipoenda kwenye kura ya wazi wakavutana siku 40, huku Ukawa wakiwa na nia kwamba walio wengi watawakatalia, lakini walipoambiwa wapeni kura ya siri hao Ukawa wakaenda kupiga ya wazi na kuwalazimisha watu wao wapige ya wazi.
Mwigulu aliendelea kufafanua, wakaenda kwenye hatua nyingine ambapo Ukawa walidai Hati ya Muungano, na kwamba walishapanga na kuwaandaa wananchi  wakidhani hati hiyo haipo ili watumie hicho ni kigezo cha wao kutoka kwenye mchakato huo.
Aliendelea kusema walipoona hilo nalo wameshindwa  na baada ya hati kutolewa, wakakosa sababu na sasa wamekuja na  hiyo ya kutoka nje na kuwaomba Watanzania kupima  wenyewe.
“Niwaombe Watanzania pimeni wenyewe… kikanuni tumeweka Kamati ya Maridhiano ambayo jambo tusiporidhiana tulipitishe kwenye kamati hiyo, na   sisi  wenyewe wabunge  tumeomba muda mrefu tuchangie wote na Mwenyekiti amesema wachangiaji ni wengi.
“Wao wamesema hapa hakuna dalili za kupiga kura bila hata kutumia Kamati ya Maridhiano au hata kuleta hapa kusema sisi hatukubali au haturidhiki na uamuzi huo, sasa Watanzania waone kama wangekataliwa au laa lakini walichokuwa wanatafuta ni namna ya kukwamisha mchakato tangu siku nyingi”, alisema Mwigulu.

No comments: