RAIS KIKWETE AKABIDHIWA TUZO YAKE YA KIMATAIFA

Rais Jakaya Kikwete amekabidhiwa rasmi Tuzo yake ya Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa zaidi katika Maendeleo Barani Afrika kwa Mwaka 2013 na kusema sio yake binafsi, ila ni ya Watanzania ambao kwa kushirikiana na uongozi wake, ndio wamefanikisha kuonekana, kutambuliwa na kuthaminiwa.
Alikabidhiwa tuzo hiyo jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe aliyeipokea kwa niaba yake,  Aprili 9, mwaka huu katika hafla iliyofanyika mjini Washington, Marekani.
Tuzo hiyo ya heshima imetolewa na jarida maarufu la kimataifa la African Leadership Magazine Group. Hutolewa kwa viongozi wa Afrika, ambao hutoa mchango mkubwa zaidi wa kiuchumi na kijamii kila mwaka kwa wananchi wao.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa, Kikwete alisema amepokea tuzo hiyo kwa moyo mkunjufu na ni  ya Watanzania.
“Mimi nimetambulika kama kiongozi lakini mafanikio haya yametokana na kushirikiana na Watanzania wote kujiletea maendeleo na mafanikio hayo yameweza kuonekana, kutambulika na kuthaminiwa. Ninachoomba Watanzania wenzangu tuendelee kushirikiana kwa sababu kumbe ushirikiano wetu umesababisha kuonekana duniani…kwani hii ni Tuzo yetu sote nawakabidhi Watanzania maana ni ya wote na si yangu binafsi,” alisema.
Waziri Membe alisema Rais Kikwete ni kiongozi wa tatu Afrika, kupata tuzo hiyo. Viongozi wengine waliokwishapata tuzo hiyo ni Rais wa Liberia na Rais wa Sierra Leone.
Kwa mujibu wa Membe, wasomaji 400,000 walipiga kura kupata mshindi wa tuzo hiyo na Rais Kikwete alichaguliwa kuwa Kiongozi wa Afrika wa kupigiwa mfano, kutokana na mafanikio katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya afya, miundombinu na elimu.
Mbali na tuzo hiyo, pia alimkabidhi Rais cheti cha kutambuliwa kilichotolewa na Wabunge weusi wa Jimbo la Georgia, Marekani kutambua mchango na mafanikio ya Rais Kikwete katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wake na Afrika kwa ujumla.
Membe alimweleza Rais kuwa hafla hiyo pia ilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, kundi la Wabunge wa Jimbo la Georgia, Watanzania waishio Marekani, viongozi wa Chama Marekani na viongozi wa Diaspora.

No comments: