POLISI DAR WAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO PASAKA

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku disko linalohusisha watoto maarufu kama disko toto  kutokana na kubaini kumbi mbalimbali hazina sifa zinazokidhi viwango vya usalama.
Kamanda wa kanda hiyo, Suleiman Kova alisema jana jijini Dar es Salaam, “kutokana na sababu za kiusalama na matishio mbalimbali katika Ukanda wa Afrika Mashariki, polisi tumepiga marufuku disko toto katika kumbi mbalimbali kutokana na sifa za kumbi hizo kutokidhi viwango vya usalama.”
Alisema katika kuhakikisha kunakuwa na usalama katika kusherehekea sikukuu ya Pasaka, kutakuwa na doria katika maeneo yote ya mikusanyiko hususani makanisani. Alitaka wananchi kutoa taarifa  wakiona dalili za uvunjifu wa amani.
Wakati huo huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alihadharisha  wananchi kwa kutaka wawe makini katika suala zima la usalama wa maisha na mali zao kwenye kipindi cha Sikukuu ya Pasaka.
Imesema uzoefu unaonesha katika kipindi cha sikukuu, wapo baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu. 
Maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka yanaanza leo kwa ibada ya Ijumaa Kuu ikiwa ni kumbukumbu ya kuteswa na kufa kwa  Yesu Kristo kabla ya kufufuka Jumapili ya Pasaka.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji wa polisi, Advera Senso, imeeleza kwamba  ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Kwa upande wa wamiliki wa kumbi za starehe, wametakiwa kuzingatia  uhalali na kuingiza watu kulingana na uwezo badala  ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.

No comments: