EAC YASHAURI TANZANIA KUBAKI IMEUNGANA

Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)  zimesihi Tanzania kubaki na muungano, zikisema uwepo wake ndiyo mwanzo na mwendelezo wa muungano wa Afrika.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed  alisema jana mjini Zanzibar kwamba kutokana na mjadala juu ya muundo wa muungano unaoendelea katika Bunge Maalumu la Katiba, baadhi ya viongozi wa  Afrika Mashariki wamekuwa na wasiwasi juu ya hatma ya muungano.
Mohamed alisema hayo wakati akifungua Kongamano la Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, lililoandaliwa na Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Alisema amekuwa akipata simu nyingi kutoka kwa viongozi wa nchi za Afrika Mashariki wakionesha wasiwasi wa kuvunjika kwa Muungano  ambao katika historia ni mwanzo na mwendelezo wa muungano wa nchi za Afrika.
Bila kutaka viongozi aliozungumza nao, alisema wamebainisha kuwa kutokana na Muungano, hata katika mikutano ya kimataifa kukiwa kuna jambo, Tanzania ikiingilia kati, kunakuwa na heshima kubwa.
“Wenzetu wanatuasa kuwa kwa namna yoyote tunayofanya katika mjadala wa Katiba mpya wa muundo wa serikali lazima tuhakikishe tunakuwa na  Muungano imara na madhubuti,” alisema.
Hata hivyo aliwaondolea Watanzania hofu akitaka wasiwe na wasiwasi na malumbano yanayoendelea katika  Bunge Maalumu la Katiba, akisema ni sehemu ya mapito kwa nchi zote na ana matumaini itapatikana katiba bora.
“Hakuna mchakato wa katiba ulio rahisi, lazima unakutana na changamoto kama tunazopitia sasa katika bunge letu maalumu, lakini nawahakikishia kuwa katiba bora itapatikana kutokana na kuwa mapito hayo ni sehemu ya kupata katiba hiyo,” alisema.
Aliwataka watanzania wanapoona wajumbe wa bunge hilo wanaenda nje ya mstari ni vema kuwakemea kwani katiba ni kwa maslahi ya Watanzania wote na ikiwa mbovu itatia nchi kwenye matatizo.
Alisema hayo wakati akitoa mwito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuchangamkia biashara kwenye masoko ya kimataifa ili kukuza uchumi wa nchi hizo.
Akiwasilisha mada kuhusu historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ushiriki wa Jamhuri ya Muungano, Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama wa Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Steven Mbundi alisema hata Umoja wa Ulaya (EU) walijifunza mambo mengi kutoka katika jumuiya iliyovunjika mwaka 1977.

No comments: