VIONGOZI WA DINI LINDI, MTWARA 'KUFUNDWA' GESI THAILAND

Viongozi 19 wa dini kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wanatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Thailand kuhudhuria mafunzo ya gesi asilia na mafuta.
Ziara hiyo inatokana na juhudi za serikali katika kuhakikisha elimu kuhusu masuala ya gesi asilia na mafuta inatolewa kwa wananchi wa kada mbalimbali ili waweze kufahamu mchakato mzima wa upatikanaji wa gesi asilia na mafuta, faida zake katika nyanja za kiuchumi na kijamii, changamoto zake na namna nchi nyingine zinavyotumia rasilimali hiyo katika kukuza uchumi.
Akiwaaga viongozi hao kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara hiyo, Mrimia Mchomvu alisema wizara imeratibu mafunzo hayo ili kujenga uelewa kwa viongozi hao ambao nao wataitumia elimu hiyo katika kuwaelimisha wananchi kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini.
Alisema Serikali imeamua kuwapeleka viongozi hao nchini Thailand kwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na kujipanga vizuri katika kutumia gesi asilia katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kuhakikisha wananchi wanafaidika na uwepo wa gesi hiyo.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Shekhe Said Sinani akizungumza kwa niaba ya wenzake, aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kushirikisha viongozi wa dini katika masuala mbalimbali ya kitaifa.

No comments: