KINGUNGE AKERWA NA WANAOMSHAMBULIA JAJI WARIOBA

Mwanasiasa mkongwe na Mjumbe wa Bunge wa Bunge Maalumu, Kingunge Ngombale-Mwiru, amesema si halali kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko, Jaji Joseph Warioba na ameonya wanaotoa lugha chafu dhidi yake, wasitumie Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama kinga yao.
Amesema CCM ni chama chenye adabu tangu kilipoanzishwa na mtu anayekitumia vibaya, kumshambulia Warioba au mjumbe mwingine yeyote, anakitukana chama kinachoongoza Serikali na wanachama wote.
“Mimi sitakubali na si halali kumshambulia Warioba au mjumbe mwingine yeyote binafsi, na tunapofanya hayo tusitumie kama ni msimamo wa CCM,” alisema Kingunge jana bungeni mjini hapa alipokuwa akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba kuhusu Sura ya Kwanza na ya Sita.
Katika majadiliano ya vikao vya Bunge hilo maalumu, wajumbe kadhaa hasa wa CCM walitoa lugha kali dhidi ya Warioba, wengine wakimtaka afunge mdomo kazi yake imekwisha, wakimwita mpiga debe, mwongo na mwenye nia mbaya na muungano.
Alisema kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba si uamuzi wa mwisho hivyo wajumbe hawana sababu ya kumtukana au kumkejeli mtu yeyote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na pia alitumia fursa hiyo kukemea lugha za matusi, vijembe na kejeli zilizotumiwa na baadhi ya wajumbe kwenye mijadala.
“Hatuwezi kukaa hapa ndani kwa kudhalilishana wale waliokuwa wakitumia lugha hizo walikuwa wanatudhalilisha wote, wengine walitumia lugha hizo kwa waasisi wetu… Unyenyekevu ni sura moja ya msomi ambaye ametumia fedha za Watanzania kupata elimu yake,” alisema.
Kingunge alisema wajumbe wamekwenda bungeni kuwatafutia wananchi wenzao Katiba mpya iliyo bora ambayo ni lazima izingatie miaka 50 ya muungano wenye mafanikio makubwa.

No comments: