BALOZI IDDI ASIKITIKIA FEDHA NA MUDA UNAOCHEZEWA BUNGENI

Wakati Bunge Maalumu la Katiba lililoketi kwa siku 70 likiahirishwa ili kupisha Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuanza Mei 6 mwaka huu, Mjumbe wa Bunge hilo, Balozi Seif Ali Idd amesikitikia muda na fedha, vinavyochezewa na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo.
Aidha, amewataka kuonea huruma fedha za walipa kodi zinazotumika na kuwashauri wajikite katika kazi iliyowapeleka pindi watakaporejea kumalizia kazi ya kuichambua Rasimu ya Pili ya Katiba, kwani Rais Jakaya Kikwete ameridhia nyongeza ya siku 60 ya vikao vya Bunge hilo linalotarajiwa kurejea Agosti 5, mwaka huu.
Balozi Idd ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, aliyasema hayo jana alipozungumza na wajumbe wa Bunge hilo bungeni mjini hapa, huku akiwasisitizia wajumbe wajiandae kuwapatia Watanzania Katiba iliyo bora.
Alisema wajumbe wamekaa kwa takribani siku 70, lakini kutokana na mvutano uliokuwepo, kazi ya kutunga Katiba haikuweza kumalizika na kusababisha Sitta kumwandikia barua Rais Kikwete ili aridhie kuongeza siku na kuongeza kuwa, siku zilizoongezwa zinapaswa kutumika vizuri.
“Serikali imetengeneza ukumbi mzuri kwa ajili ya kujadili Katiba, waliotoka nawasihi warudi, Katiba haitungwi barabarani wala katika mikutano ya hadhara, ni humu ndani, nawasihi warudi tuendelee na mchakato, Serikali imetumia fedha nyingi na inaendelea kutumia.
“Jana (juzi) Waziri wa Fedha (Saada Mkuya) alisema hapa kwamba kwa siku tunatumia Sh milioni 188, sasa fikiria siku 70 zaidi ya Sh bilioni 20 zimetumika mpaka sasa na hatukumaliza kazi kwa siku hizo, tulitumia muda mwingi kwenye kutunga kanuni na mfumo wa kura, wazi na siri,” alisema Balozi Seif Idd.
Alisema ni baada ya yeye na Waziri Mkuu Pinda, kukutana na pande zilizovutana kuhusu mfumo wa kupiga kura bungeni humo ndipo ikaridhiwa aina zote zitumike, na ndipo kuanza kujadili sura mbili pekee, ya kwanza na ya sita. Aliwataka wajumbe kuzionea huruma fedha za walipa kodi.
Naye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na wajumbe hao na kwa nyakati tofauti, pamoja na mambo mengine aliwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliotoka bungeni wiki iliyopita, kurejea Agosti kuendelea na mchakato.
Akitumia msemo; `Yaliyopita Si Ndwele, Tugange Yajayo’, aliungana na wajumbe wengine waliowasihi wajumbe wa bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) warejee bungeni, akiwataka warejee kwa kuwa wamegoma katika hatua za mwanzo wakati Katiba yoyote kazi kubwa ipo katika kuiboresha mwaka hadi mwaka.
Aidha, alisema Tanzania ni nchi pekee yenye muungano uliofanikiwa na wa kuigwa na nchi nyingine zimejaribu lakini zimeshindwa hivyo kuukejeli muungano ni kujivunjia heshima.
“Huu ni muungano wa nchi mbili, Zanzibar na Tanganyika, ni muungano usiofananishwa na nchi nyingine, umejengwa katika mahusiano ya kabla ya muungano na kama si sababu za historia ya Ukoloni, leo tungezungumzia nchi moja,” alisema Pinda.
Kwa mujibu wa Pinda, wanaodai Tanganyika yao, haipo kwa kuwa ilidumu kwa mwaka mmoja na nusu pekee, kisha ikaungana na Zanzibar na wakati wa muungano yeye alikuwa na miaka 16 na kuhoji anayetaka Tanganyika, ni ipi hiyo?
Pinda alisema kwa kuukejeli na kuudharau muungano pamoja na waasisi wake, ni jambo la kukera na kama Mwalimu Nyerere (Julius Kambarage) angekuwepo leo, kwa waliomtukana angesema Mungu wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.
“Mwalimu si mtu wa kubeza kwa kiasi hicho, dunia nzima inamheshimu, ukombozi wa nchi nyingi za Afrika hasa Kusini aliuwezesha yeye, leo kijana wa juzi anatoa lugha mbovu kwa mzee huyu? Nikasema eeeh! Ipo kazi,” alisema Pinda jana akizungumza na wajumbe wa Bunge hilo.
Alisema kero za muungano zilikuwa zaidi ya 20, lakini leo zipo sita na zinashughulikiwa hivyo kusema kila kukicha zinaongezeka si kweli.
Kuhusu Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na kuwasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kama mapendekezo, Pinda alisema hakuna kipya kwa kuwa masuala ya utawala, mahakama, bunge yataendelea kuwepo ila kwa mfumo ulioboreshwa.
Naye Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta aliliahirisha Bunge hilo jana, mjini hapa baada ya kuwahoji wajumbe ili kupitisha majadiliano ya Sura hizo mbili kupelekwa katika Kamati ya Uandishi kabla ya kuamuliwa Agosti Bunge litakaporejea.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Amir Kificho, alikanusha kuwa yeye na Baraza la Wawakilishi walitaka serikali tatu na kusema jambo hilo halijawahi kutokea na halitakaa litokee.
“Wajibu wetu kuwapatia wananchi Katiba bora si kwa Watanzania pekee hata kwa Mungu, maoni ya kuchanganya yalitolewa kuwa Baraza la Wawakilishi, Kificho tunataka serikali tatu, haijatokea na haitakaa itokee, naomba wananchi waamini ninachosema sasa mdomoni mwangu, mimi ni muumini wa serikali mbili zilizoboreshwa,” alisema Kificho.
Alitaka marekebisho yafanyike ili ziendelee kutumika kwani hali ya uchumi, amani na utulivu iliyopo si ya kujaribu serikali tatu bali kuendelea na serikali mbili.
Awali, Sitta alifafanua kuhusu tuhuma mbalimbali zilizotolewa kwa kiti chake kuwa ameachia matusi na vurugu bungeni wakati kanuni zinaruhusu achukue hatua za kutumia hata nguvu, na kusema aliacha ili wananchi wajue na kuona nani anafanya nini.
“Tena wajumbe tuliongezewa askari wa Bunge hapa, lakini sikuona sababu ya kutumia nguvu kwa kuwa nilitaka wananchi wajue wajumbe wanafanya nini, na nani yukoje,” alisema Sitta.
Alisema pia kuwa, alituhumiwa kubagua kuwatembelea viongozi wa dini, na kusema ni ziara endelevu, atawatembelea viongozi sio wa dini pekee bali hata taasisi na makundi mengine.
Kwa takribani siku 70, Wajumbe wa Bunge hilo 629 walikuwa katika majadiliano ya sura mbili, ya Kwanza na ya Sita baada ya kutumia zaidi ya siku 40 kutunga kanuni na kupitisha mfumo wa upigaji kura uliokumbwa na mvutano mkali kuhusu kura ya siri ama ya wazi.
Bunge Maalumu la Katiba limeahirishwa jana hadi Agosti 5 mwaka huu, kupisha Bunge la Jamhuri ya Muungano la Bajeti na Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa ajili ya kikao cha bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015.

No comments: