TWB KUTOA MIKOPO YA VIWANJA KWA WANAWAKE

Benki ya Wanawake (TWB) imebuni mpango wa kuwainua wanawake wajasiriamli, kwa kuwapatia viwanja vilivyopimwa kisheria vyenye hati miliki ili kuwawezesha kukopesheka kirahisi.
Mpango huo unatokana na benki nyingi nchini kuwa na masharti magumu kwa wanawake wanaojishughulisha na ujasiriamali, kwa kuwataka kuwa na mali isiyohamishika yenye hati miliki kama vile viwanja na nyumba ili kuweza kukopeshwa fedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa TWB,  Magreth Chacha alisema lengo la mpango huo ni kuwainua wanawake kwa kuwakopesha viwanja ili waweze kuinuka kiuchumi, kwani watapata mikopo kirahisi na kulipa kidogo kidogo hadi watakapomaliza mikopo yao.
Alikuwa akizungumza katika mafunzo kwa wafanyakazi wa benki hiyo, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuwahudumia wateja katika mazingira mazuri na kuhakikisha wanawapa wateja kipaumbele katika kupata huduma za kibenki na kwa wakati.
"Mpango huu utatuwezesha kutoa mikopo kwa wanawake wajasiriamali nchi nzima, hata kule ambako hatuna matawi kwani tumeungana na benki nyingine ambazo zitatusaidia kuwezesha wanawake hao kupata mkopo wa viwanja," alisema.
Alitoa mwito kwa wanawake wajasiriamali kuitumia fursa hiyo ili waweze kupata viwanja na kujenga nyumba, ambazo zitatambulika kisheria na ambazo zitakuwa na hati zitakazowasaidia  kukopesheka benki na kuondokana na vikwazo vinavyodumaza ukuaji wa uchumi wao.
"Tutashirikiana na Kampuni wa upimaji viwanja ya Ardhi Plan ya Dar es Salaam, ambayo itahusika katika kupima viwanja katika maeneo mbalimbali nchi nzima, o wataanza kwa awamu katika mpango mzima wa kuwafikiwa wakina mama wa nchi nzima," alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo na Huduma kwa Wateja cha Benki hiyo, Yebete Zabron alisema mafunzo waliyoyapata, yatawasaidia katika kuboresha huduma kwa wateja.

No comments: