KAMPUNI ZAHIMIZWA KUUNGANA KUZUIA MALARIA

Kampuni mbalimbali  zimehimizwa kuungana katika juhudi za kuzuia na kutibu malaria kupitia mkakati wa pamoja , ujulikanao kama Malaria  Safe Initiative.
Mkakati huu unalenga kuhamasisha sekta binafsi, hasa kampuni kujishughulisha na juhudi za kupambana na ugonjwa huo katika maeneo yao ya kazi, familia za wafanyakazi na jamii inayowazunguka.
Ofisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, Pratap Ghose alisema wadau katika sekta binafsi wana nafasi muhimu na ya kipekee kufanikisha mapambano dhidi ya malaria.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Malaria duniani jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Ghose ambaye kampuni yake imejiunga na mkakati huo, alisema wamesambaza vyandarua kwa wafanyakazi wake zaidi ya 500.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alipongeza kampuni na washirika wa maendeleo kwa juhudi zao za kupambana na malaria.
Dk Seif  alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, nchi imeshuhudia kupungua kwa kasi ya maambukizi ya malaria kwa asilimia 50, kutoka asilimia 18 mwaka 2007/08 hadi asilimia tisa mwaka 2011/12.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Sharon Cromer alisema malaria itatokomezwa pale tu wadau kutoka sekta mbalimbali watakaposhirikiana.

No comments: