SHULE IKO TAABANI, WALIMU WAISHI KWENYE DARASA

Shule ya Msingi Mwamashimba katika Kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu Shinyanga, inakabiliwa na ukosefu wa vyoo, madawati na nyumba za walimu, hali inayosababisha baadhi ya walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa.
Waandishi wa habari  walitembelea shule hiyo,  kutaka kufahamu  wanafunzi wanapataje elimu kupitia vyumba hivyo na mazingira yaliyopo  na  wakihoji baadhi ya viongozi.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Elias Zengo alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1976, ina jumla ya wanafunzi 492 na walimu tisa, ambapo wa kike ni mmoja.
Alitaja changamoto zinazokabili shule hiyo kuwa ni upungufu wa vyumba vya madarasa na  ukosefu wa vyoo vya wanafunzi.
Tatizo lingine ni nyumba za walimu,  ambapo kwa sasa kuna nyumba mbili tu, hali inayowafanya baadhi ya walimu kuishi kwenye vyumba vya madarasa.
Shule haina vyoo, hali inayowafanya wanafunzi kutumia choo, ambacho ujenzi wake haujakamilika baada ya kukwama muda mrefu. Upungufu wa madawati, umesababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Mwamashimba ilipo shule hiyo, alikiri kuwepo kwa changamoto hizo.
Alisema wanajiandaa kufanya mkutano na wananchi ili kuangalia namna ya kuzitatua, kama vile kuchanga pesa kujenga nyumba za walimu.

No comments: