ABIRIA WA BODABODA APIGWA RISASI TABATA MATUMBI

Mtu mmoja ambaye hajafahamika, aliyekuwa amepakiwa kwenye pikipiki, amejeruhiwa kwa kupigwa risasi mguuni.
Abiria huyo ambaye jina lake halikupatikana, anadaiwa kupigwa risasi na askari wanaolinda Benki ya Acess, iliyopo eneo la Tabata Matumbi barabara ya Mandela jijini Dar es Salaam.
Mashuhuda ambao walizungumza na mwandishi, walisema abiria huyo alikuwa amepakiwa na mwendesha pikipiki, ambaye alikuwa ameegesha pikipiki hiyo eneo la benki hiyo.
"Pikipiki ya wale jamaa ilikuwa imepaki nje ya benki, lakini wakati tunaendelea na maongezi hapa, ghafla tukasikia mshindo mkubwa, tukadhania kuwa ni tairi la gari limepasuka, lakini ghafla tukamuona huyu mtu akija ana jeraha mguuni," alisema mmoja wa watu waliokuwepo eneo hilo.
Aidha, mwendesha pikipiki katika eneo hilo, alisema alimuona mtu huyo akija upande wao akiwa na jeraha huku akidai askari ndiyo wamempiga risasi.
Alisema wakati mtu huyo akiwa eneo hilo, anaugulia maumivu ya risasi, ghafla walifika askari na kumkamata kisha kuondoka naye.
"Hatuna uhakika kama ni kweli askari ndiyo wamempiga, lakini askari walifika hapa na kuwakamata wote wawili, dereva na abiria wakaondoka nao," alisema mtu huyo.
Mwandishi alijaribu kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi ili afafanue tukio hilo. Alisema bado ni mapema hivyo atafuatilia kubaini tukio hilo.

No comments: