AJALI ZAUA WATU SABA WILAYANI BUNDA

Watu saba wamekufa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali za barabarani  na majini wilayani Bunda Mkoa wa Mara.
 Kwa mujibu wa Polisi, ajali hizo ni za juzi na jana, ambapo ya kwanza ni ya gari ndogo aina ya Noah, yenye namba za usajili  T 258 BRB katika eneo la Barabara kuu ya Mwanza-Musoma.
Gari hilo lilimgonga Mwenyekiti wa Kijiji cha Kunzugu, Vicent Magesha aliyekufa papo hapo, huku abiria aliyekuwa amempakia, alinusurika bila kupata majeraha.
Ajali ya pili  ni ya juzi usiku katika eneo la Serengeti kwenye barabara hiyo. Ilihusisha gari aina ya Fuso lenye namba  T 437 AKN, lililokuwa likitoka mnadani  Dutwa wilayani Bariadi kuelekea mjini Bunda.
Katika ajali hiyo, Daniel Boniphace (30), mkazi wa mjini Bunda, alikufa papo hapo na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa vibaya.
Polisi walisema chanzo cha ajali hiyo ni kundi kubwa la wanyama aina ya nyumbu, waliokuwa wanatoka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kukatiza barabarani ghafla. Dereva alipojaribu kukwepa wanyama hao, gari liliyumba na kuanguka.
Waganga wa zamu katika wadi ya wanaume na wanawake, katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda,  walitaja majeruhi kuwa ni  Gerald Hamenya (30), Chigwenyi Musimu (40), Mkami Munanka (20), Duta Pinu (35), Mwita MungÕare (26), Njire Zanzibar (33), Robert Fabian (31), Gerald Gurani (37), George Natusi (30) na James Mungine (16), wote wakazi wa wilayani Bunda.
Wengine ni Stephen Segese (16), Juma Julius (37), Ezekiel Julius (31), James Lwala (45), Makoba Maduhu (23), Magdalena Farancis (35), wote ni wakazi wa mjini Bunda na Roda Paul (18), mkazi wa Musoma.
Wengine ni Anastazia Nyarari (45), Mariam Tega (39), Joyce Jackson (28), Giradis Laurent (38), Wakuru Makanga (36), Ripa Munigu (41), Wiliada Mato (52) na Agnes Mwita (40), wote  wakazi wa wilayani hapa.
Ajali nyingine ni ya jana asubuhi katika eneo la Tairo, ambapo Hiace yenye namba za usajili T. 521 CSU mali ya Rukanga Charles, iliyokuwa inaendeshwa na Shimba Wilson, mkazi wa mjini Bunda, ilimgonga mwendesha pikipiki, Safari Hamisi (35) aliyekufa papo hapo  pamoja na abiria wake, Nyanjige Magafu Kaboja (35) aliyekufa muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini. Wote ni wakazi wa kijiji cha Guta.
Ajali nyingine ni ya mtumbwi, uliozama Aprili 16 mwaka huu  usiku  katika Ziwa Victoria eneo la kijiji cha Isanju Kata ya Iramba.
Katika ajali hiyo, baba na mtoto wake walikufa maji baada ya mtumbwi wao kupigwa na dhoruba, iliyoambatana na mvua kubwa.
 Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iramba, Marko Mabula, alitaja watu hao kuwa ni Kanywagale Mkangara (61) na mtoto wake, Mtaki Boma Kanywagale 36), wote wakazi wa kijiji cha Isanju wilayani hapa.
 Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ferdinand Mtui hakupatikana jana kuzungumzia matukio hayo. Lakini, polisi wilayani hapa walithibitisha. Walisema chanzo cha ajali za barabarani ni mwendo kasi wa madereva.

No comments: