RAIS KIKWETE ATUNUKU NISHANI, TUZO YA MUUNGANO

Rais Jakaya Kikwete ametunuku nishani na kutoa tuzo za Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Muungano kwa watu 8,6 wakiwemo viongozi walioingia madarakani kikatiba na wameendelea kuonesha maadili mema na kuwa mfano wa kuigwa kwa kipindi hicho kwa uaminifu.
Sherehe hizo zilifanyika juzi usiku Ikulu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali  na mabalozi wa nchi mbalimbali.
Miongoni mwa waliotunukiwa nishani ni pamoja na waasisi wa Muungano, Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Shekhe Abeid Amaan Karume.
Pia wamo marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili na Benjamin Mkapa aliyeongoza Awamu ya Tatu.
Wengine waliotunukiwa Nishani Daraja la Kwanza ni  Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, Mawaziri Wakuu wa Tanzania ambao kwa nyadhifa zao pia walikuwa Makamu wa Rais, Rashid Kawawa, John Malecela, Cleopa Msuya na Jaji Joseph Warioba, ambaye mpaka hivi karibuni alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Nishati hizo zimetolewa pia kwa Makamu wa Rais mstaafu, Dk Omar Ali Juma, Idrissa Abdulwakil, Rais wastaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour Juma na Amani Abeid Karume.
Nishati Daraja la Pili ilikwenda kwa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, Baraza la Mawaziri wa Tanganyika wa mwaka 1964 na viongozi wastaafu walio hai au marehemu, ambao walitetea Muungano na kuendelea kuonesha maadili mema hata baada ya utumishi wao.
Watu hao ni waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Sokoine, Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye, Brigedia Jenerali Ramadhani Haji Faki, Shamsi Vuai Nahodha, Thabit Kombo Jecha, Seif Bakari Omari, Meja Jenerali Abdallah Said Natepe, Brigedia Jenerali Yussuf Himid Maftah, Hafidhi Suleiman Almasi na Khamis Darwesh Mdingo.
Wengine ni Pili Khamis Mpera, Said Iddi Bavuai, Said Washoto Mnyuke, Hamid Ameir Ali, Meja Jenerali Khamis Hemed Nyuni, Mohammed Abdallah Ameir, Edington Hebert Kisasi, Hasnu Makame Mwita, Mohammed Juma Khamis, Mohamed Mfaume Omari, Muhsin Bin Ali Juma, Daudi Mahmoud Jecha, Asanterabi Wai, Paul Bomani, Habib Amir Jamal, Lawi Sijaona, Said Ali Maswanya, Jeremiah Kasambala, Tewa Tewa na Solomon Eliufoo.
Katika kundi hilo, wamo pia Clement Kahama, Job Lusinde, Dereck Bryceson, Austin Shaba, Amri Abeid Kaluta, Chifu Adam Sapi Mkwawa, Ali Khamis Abdallah, Augustino Said, Augustino Ramadhani, Dunstan Omar, Dickson Nkembo, Makame Suleiman, Suleiman Ali Mnoga, Mark Bomani na Iddi Pandu Hassan.
Nishani Daraja la Tatu ilitunukiwa kwa wakuu wa vyombo vya ulinzi walioko madarakani au waliostaafu, mawaziri na viongozi waandamizi wastaafu ambao walionesha maadili katika utumishi wao na hata baadaye, ambao ni Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Minja,  Zakhia Meghji, Mirisho Sarakikya, Abdallah Twalipo, David Musuguri, Elangwa Shaidi, Hamza Aziz Ali, Samwel Pundugu, Obadia Rugimbana na Ramadhani Nyamka.
Kwa upande wa Nishati Daraja la Nne, ilitolewa kwa wake wa marais waasisi wa Muungano, Maria Nyerere na Fatma Karume. Wengine ni waliochanganya udongo wa Muungano Hassan Omari Mzee, Hassaniel Mrema, Sifael Shuma na Khadija Abbas. Wengine waopewa nishani hiyo ni Vicky Nsillo-Swai na Ali Mwinyikondo Mwinyigogo.
Aidha, Rais Kikwete aliitoa nishati kwa Bruda Anthony Canterucci na Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency, Dk Rajan Kanabar. Pia, Rais Kikwete alitoa tuzo kwa raia wa Tanzania na kigeni ambao  wametoa mchango muhimu katika huduma za kijamii nchini ambao ni Mark Green, Hayao Nakayama na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Rais alitunuku nishani na kutoa tuzo hizo kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Rais Sura ya 9, kama ilivyofanyiwa Marekebisho  mwaka 2002  Fungu la 4, kama ilivyotangazwa katika Tangazo la Serikali Namba 114 la Aprili 24.

No comments: