KANUNI SABA ZA BUNGE MAALUMU LA KATIBA ZAREKEBISHWA

Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum imezifanyia marekebisho Kanuni zake Saba kwa lengo la kuweka utaratibu mzuri wa wajumbe kupendekeza marekebisho ya ibara na sura mpya za Rasimu ya Katiba.
Hayo yalielezwa bungeni mjini hapa jana na Mjumbe Bunge hilo, Evod Mmanda wakati alipokuwa akiwasilisha Azimio la kufanya marekebisho ya kanuni za Bunge Maalumu kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati ya hiyo.
Mabadiliko yaliyopendekezwa ni orodha ya yaliyomo, kanuni ya 32,33, 35,41, 60, 62 na 82.
Mabadiliko hayo yametokana na kutokuwepo kwa maelezo ya wazi ya namna Kamati ya Uandishi itakavyotekeleza kazi baada ya mjadala wa sura za Rasimu ya Katiba kuhitimishwa.
Mmanda alisema, kamati hiyo imefanya marekebisho katika kanuni ya 41 ambayo yametokana na kutofautiana kwa fasili za kanuni ya 41 ambapo dhana inayoelezwa katika kanuni hiyo ni hoja ya kuwasilisha Rasimu ya Mwisho ya katiba.
Marekebisho mengine yaliyofanywa na kamati hiyo ni katika kanuni ya 60(a) na 62(2) kwa ajili ya kurekebisha kasoro, zilizojitokeza kwa kutozingatia kurekebisha baadhi ya kanuni, ambazo zilihitaji kurekebishwa kufuatana na marekebisho ya kanuni nyingine.
Alitaja miongoni mwa makosa hayo kuwa ni pale Bunge Maalum, lilipofanya marekebisho ya kanuni 32 ili kuruhusu kamati ya uongozi kupanga zaidi ya sura mbili za Rasimu ya Katiba kujadiliwa na kamati.
Hata hivyo, Mmanda alisema baada ya kurekebishwa kwa kanuni hiyo ya 32, bado kanuni nyingine kama vile kanuni ya 60(a) na 62(2) zilibaki na dhana ile ile ya kamati kujadili sura mbili tu za Rasimu ya Katiba.
Sambamba na kanuni hizo kanuni nyingine iliyorekebishwa ni ile ya 82 ambayo imetokana na  kuwepo kwa tofauti katika baadhi ya fasili za kanuni hiyo.
Alisema wakati fasili ya (9) inaweka mavazi yanayoruhusiwa kwa wajumbe wa Bunge Maalum, fasili ya (7) na (8) zinatambua kuwepo kwa neno vazi rasmi kwa wajumbe.
Aliongeza kuwa marekebisho ya kanuni hiyo, yanakusudia kufuta maneno ya vazi rasmi yaliyopo katika fasili ya (7) na (8) ya kanuni ya 82 na badala yake kuweka maneno ‘Vazi linaloruhusiwa’ ili kuleta mantiki katika kanuni hiyo.

No comments: