MAJAMBAZI WAVAMIA WACHINA WANAOJENGA BARABARA

Watu wanane  wanaosadikiwa kuwa  majambazi  wakiwa na silaha za  jadi  yakiwemo  mapanga na marungu, wamevamia  kambi  ya Kampuni  ya Wachina.
Wachina hao ni wale wanaojenga  barabara inayounganisha  Mji wa Mpanda wilayani Mpanda   na Kijiji cha Sitalike wilayani Mlele Mkoa wa Katavi  na kumjeruhi vibaya  mlinzi wa kampuni hiyo.
Kamanda  wa Polisi  wa Mkoa  wa Katavi, Dhahiri Kidavashari  akizungumza na mwandishi  wa habari  hizi kwa njia ya  simu,  alisema  tukio  hilo  lilitokea Aprili 22 mwaka huu, saa 5:35  usiku  katika  kambi ya kampuni  hiyo ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami,   iliyopo Kijiji cha  Magamba  wilayani  Mlele.
Alisema  siku  hiyo ya  tukio,    majambazi hao  walifika kambini hapo  na kumvamia  mlinzi huyo,  Joseph Sarangi  na kumkatakata  kwa  mapanga  na  kumpiga kwa  marungu. Sarangi amejeruhiwa vibaya usoni  na kichwani.
Kamanda  Kidavashari  alisema majambazi hao waliiba  betri  ya  gari  aina ya  Nissan  yenye  Namba  12, kisha kutokomea kusikojulikana.
Alisema Polisi walifanya  msako  mkali kuhusiana na tukio hilo na walimkamata mtuhumiwa,  Juma Athman (23) , mkazi  wa Mtaa wa Tambukareli mjini hapa.

No comments: