MALIMA AWAFUNGA MDOMO WAJUMBE WA UKAWA

Utangulizi wa Mwalimu Julius Nyerere alioutoa katika kitabu cha Simulizi ya Thabit Kombo, kilichoandikwa na Minaeli Mdundo, umetumiwa na Mjumbe Adam Malima katika Bunge Maalumu la Katiba, kuwanyamazisha wajumbe waliowatukana waasisi wa Taifa.
Malima huku akinukuu utangulizi huo ikiwa ni majibu ya dhihaka na matusi, yaliyotolewa na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wa kundi la Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa) kwa waasisi wa Muungano, alisema heshima, utu na busara ya wazee hao, hakuna mtu yeyote leo anayeweza hata kuwa nayo kidogo.
Alitoa mfano kauli ya mjumbe wa Ukawa, Ismail Jussa Ladhu aliyowahi kuitoa akimwambia Malima bungeni humo, kwamba Rais Abeid Amaan Karume na muasisi wa Chama cha Afro Shiraz Party (ASP), Thabit Kombo ndio wajinga, lakini si Wazanzibari wa leo, alisema hizo ni kejeli na matusi yasiyovumilika.
“Mzee Kombo anazungumziwa na Nyerere katika kitabu hiki (akionesha kitabu) kuwa ni mtu mtaratibu, mwenye busara na akili nyingi ambaye katika matatizo mengi ya kisiasa yaliyowahi kutokea, walimtegemea sana kuyamaliza, huyu ndio leo hana akili?” alihoji Malima.
Alisema katika nchi mbalimbali duniani, waasisi wao ni sehemu ya Tunu ya Taifa, wanathaminiwa na kuheshimiwa lakini hapa nchini watu wanaona fahari kuwatusi.
Alisema kwa hekima na akili alizokuwa nazo Kombo, Jussa hafai kuwa hata ndala (mitarawanda) ya Thabit Kombo.
Akizungumzia posho, Malima ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, alisema baada ya kutangaza hivi karibuni kuwa serikali haitoi fedha kwa wajumbe wasiohudhuria vikao, alipokea ujumbe mfupi wa simu yake ya mkononi, ukimtusi kwamba amefanya fedha hizo ni za baba yake.
“Nimetumiwa meseji (ujumbe mfupi) Mwenyekiti kwamba nafanya kama pesa ni za baba yangu, sasa kama walikuwa wanataka fedha, mbona hawaingii ndani?” Alihoji Malima.
Alisema wananchi wanafuatilia Bunge kwa makini kwa sasa, lakini wamemwambia wanakosa uhondo wa BBM (Bongo Bunge Movie), kutokana na Ukawa aliyodai walikuwa wakifanya vituko bungeni, kutoka nje ya Bunge hilo na kususia vikao wiki iliyopita.
Alidai mjumbe Profesa Ibrahimu Lipumba, ametukana Bunge na Wajumbe wote tusi lililopitiliza kulingana na usomi wake na kumtaka afute neno la Interahamwe akiwa nje ya Bunge na arejee bungeni kulifuta vile vile.
Wiki iliyopita, akichangia hoja kabla ya kuongoza Ukawa kutoka nje, Profesa Lipumba alisema wajumbe wa Bunge hilo ni kama Interahamwe (kundi la mauaji ya kimbari Rwanda). Walipotoka nje ya Bunge, baadhi ya wajumbe wa Ukawa walisikika wakiimba Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Interahamwe. Mwenyekiti Samuel Sitta alisema katika Kamati ya Uongozi iliyokutana Alhamisi wiki hii kuwa, anaendelea kutafuta suluhu na Ukawa.

No comments: