TANZANIA YATARAJIWA KUUAGA UMASIKINI MWAKA 2025

Tanzania inatarajiwa kuondoka kwenye kundi la nchi masikini na  kuhamia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akifungua kongamano linaloendelea hapa.
Kongamano hilo ni njia mojawapo ya kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliozaa nchi mpya ya Tanzania.
Kongamano hilo linakutanisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na mabalozi, wataalamu na wafanyabiashara, ambapo  Profesa Muhongo alipata nafasi ya kuwasilisha mada kuhusiana na  fursa zilizopo katika  sekta ya  gesi, mafuta na madini.
Alisema ili nchi ya Tanzania iweze kupiga hatua kimaendeleo, inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye nishati ambayo ndiyo yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Akielezea juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na maisha  bora, alisema serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza juhudi  za kupeleka umeme kwenye vijiji vyote kwa awamu tofauti tofauti.
Profesa Muhongo aliongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa  nchi inapata umeme wa kutosha, serikali imekwishaanza mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la gesi linaloanzia Mtwara hadi Dar es Salaam.
Akizungumzia mradi huo, Profesa Muhongo alisema kuwa gesi itakayozalishwa itatumika majumbani, viwandani na kwenye magari na nyingine itauzwa nchi za jirani na kuliingizia pato Taifa.

No comments: