PINDA KUONGOZA MAZIKO YA ASKOFU WA ANGLIKANA...

Marehemu Godfrey Mdimi Mhogolo.
Wachungaji wapatao 300 waliokuwa wakifanya kazi chini ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dodoma, Marehemu Godfrey Mdimi Mhogolo wametakiwa kujipa moyo wakati wa kipindi hiki kigumu cha kumpoteza kiongozi wao.

Hayo yalisemwa jana na Msaidizi wa Askofu wa kanisa hilo, Mchungaji George Chomola wakati wa ibada ya kumuaga marehemu Mhogolo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana mjini hapa.
Mamia ya wakazi wa Dodoma na mikoa jirani, walifurika kanisani hapo kumuaga Askofu huyo ambaye anatarajiwa kuzikwa leo kwenye viwanja vya kanisa hilo.
"Nawatia moyo wachungaji 300 waliokuwa wakifanya kazi chini ya  Mhogolo wasiwe na wasiwasi na kuanza kujiuliza kwa nini amewatoka mapema kiasi hiki hivyo wamtegemee Mungu na atawapa kiongozi mwingine," alisema.
Alisema sasa jimbo hilo litakuwa chini ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob  Chimeledya.  Wageni kutoka ndani na nje ya nchi, bado wanafika kanisani hapo kutoa rambirambi zao.
Askofu Mhogolo alifariki dunia mwishoni mwa mwezi uliopita wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Milpark ya jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  anatarajiwa kuongoza ibada ya mazishi, itakayoanza leo asubuhi kanisani hapo.

No comments: