KAMATI YA WASSIRA YATAKA BARA IJIVUE KOTI LA MUUNGANO...

Stephen Wassira.
Mwenyekiti wa Kamati namba Sita ya Bunge Maalum la Katiba, Stephen Wassira amesema kamati yake imependekeza Tanzania Bara kuvua koti la Muungano, linalodaiwa kuvaliwa ili koti hilo sasa livaliwe na pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar, kama njia ya kuimarisha Muungano.

Alisema uamuzi huo ulifikiwa na wajumbe wa kamati yake, kama njia ya kukwepa kuifanya Tanzania kuwa na Muungano wa Shirikisho kama ilivyopendekezwa na rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake kutatua kero za mfumo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili.
Akielezea mwenendo wa mjadala wa kamati yake kwa waandishi wa habari jana, Wassira alisema msingi wa majadiliano katika kamati yake ulijikita zaidi katika hoja ya Muungano wa Shirikisho na Muungano wa Serikali Mbili ambapo upande wa wanaotaka Muungano wa Serikali Mbili ulishinda.
Alisema hoja iliyojengwa na waliokuwa wanataka mfumo wa Shirikisho kufuatwa ambao ungefanya Muungano kuwa wa Serikali Tatu ilikuwa ni kwamba katika kipindi cha miaka 50 Muungano umekuwa na kero nyingi.
Alisema kwa upande wa kundi linalotaka Serikali Mbili hoja ilikuwa ni kwamba pamoja na kero za Muungano zipo jitihada zinazofanywa ili kutatua kero za Muungano na kwamba kubadili mfumo kwenda Serikali Tatu hakutasaidia kuimarisha Muungano bali kutaua.
Alisema miongoni mwa kero zilizokuwa zinasababisha matatizo ni kero za kikatiba ambazo wajumbe waliona ni wakati mwafaka sasa kwa Katiba mpya kuondoa kasoro hizo ili kuimarisha Muungano.
"Hoja ya Tanzania Bara imevaa koti la Muungano ilijadiliwa na kimsingi tulikubaliana kwamba sasa ni wakati muafaka kwa koti la Muungano sasa kuvaliwa na pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar ili kuziwezesha pande zote kufaidika na Muungano.
"Kimsingi tumezingatia hoja kwamba ni mambo gani tukiyaondoa kwenye Muungano yanaweza kukidhi hoja ya Zanzibar  kwamba Muungano wa sasa unainufaisha zaidi Tanzania Bara kutokana na kuvaa koti la Muungano," alisema Wassira.
Alisema kamati yake imependekeza Zanzibar ipewe uhuru kwa mambo yanayohusu haki na mamlaka ya ndani, lakini kwa mambo yanayohusu idhini ya Muungano iweze kushirikiana na Serikali ya Muungano na manufaa yanufaishe pande zote.
Alisema katika kupiga kura kwa jambo hilo, upande wa Tanzania Bara walitimiza theluthi mbili ya wajumbe ambao waliunga mkono muundo wa Serikali Mbili lakini kwa Zanzibar idadi ya kura haikuweza kutimia theluthi mbili.
Mwenyekiti huyo alizungumzia pia majadiliano katika kipengele cha mipaka ya Tanzania, ambapo mambo kadhaa yaliongezwa kama vile kuzingatia mipaka ya ardhi, maziwa, mito, bahari, anga na kitako cha bahari.
Kuhusu Sikukuu za Kitaifa alisema Kamati yake pamoja na kuwepo kwa hoja ya kuzifanya Sikukuu kama za Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar kutokuwa za Muungano, lakini hoja hiyo ilipingwa kutokana na wajumbe wengi kutaka sherehe hizo ziwe ni za Muungano Kikatiba ili kulinda historia.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati namba Tano, Hamad Rashid Mohammed jana alijitokeza mbele ya waandishi wa habari kwa mara ya pili, safari hii akizungumzia mjadala wa Sura ya Sita ambapo alisema wajumbe wengi wamekataa Muungano wa Shirikisho na kutaka mfumo wa Serikali Mbili.
Alisema wajumbe wa Kamati hiyo walikikataa kabisa kifungu namba 60 cha Sura ya Sita kinachotamka kwamba Muungano utakuwa ni wa Shirikisho ambapo pande zote za Muungano walitimiza theluthi mbili ya kura katika kukipinga na wametoa mapendekezo mapya.
Alisema pamoja na kifungu hicho, Kamati hiyo imevikataa vifungu vingine vinane vinavyotamka kwamba Muungano utakuwa ni wa Shirikisho na hivyo yapo mapendekezo yaliyoingizwa kwenye vifungu hivyo ambayo yatawasilishwa kwenye taarifa ya kamati hiyo kwa Bunge.

No comments: