PADRI ATAKA WABUNGE KUACHA KUTETEA MASLAHI BINAFSI

Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wameshauriwa kutambua kwamba karama na uwezo waliopewa ni kwa ajili ya kuandaa Katiba mpya ya kuipeleka Tanzania kwa miaka zaidi ya 50 ijayo na siyo kujikita katika maslahi yao binafsi.
Rai hiyo imetolewa jana na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Ukonga, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padre Venance Tegete kwenye maadhimisho ya Ibada ya Pasaka katika Kigango cha Mtakatifu Monica.
‘’Kinachotufanya tuishi kama tulivyo kwa maelewano ni kutokana na misingi mizuri iliyowekwa na waasisi wa taifa hili,’’ alisema.
Alikumbusha kuwa ukiacha tukio la Tanzania kuvamiwa na Nduli Idd Amin Dadah wa Uganda (1978) na kisha kutolewa nje ya mipaka, Watanzania wamekuwa wakiishi kwa amani, utulivu na maelewano kwa kipindi chote cha miaka 50 iliyopita.
‘’Kama waasisi wa Taifa hili wangekuwa na ubinafsi, wewe na mimi tusingekuwa hapa kama tulivyo leo,’’ alisema Padre Tegete kwenye ibada iliyofurika waumini.
Alisema katika kila msafara wa mamba, kenge pia wamo hivyo kuwashauri wabunge kuwa makini katika jukumu lao kubwa na nyeti la kutunga Katiba mpya ya Tanzania.
‘’Tusiwe kama nyimbo za bongo fleva, ambazo huvuma kwa kasi mwanzoni na kisha hutoweka ,’’ alisisitiza katika mahubiri yake.
Alizikumbusha familia kuishi kwa kusameheana, upendo na umoja wa kweli ili kuleta ustawi wa jamii.
Sherehe ya Pasaka huadhimishwa na Wakristo duniani kote, kukumbuka kifo cha Yesu Kristo na kufufuka kwake miaka zaidi ya 2,000 iliyopita.

No comments: