WANAOJICHUKULIA SHERIA MKONONI WASHUTUMIWA

Mtandao wa watu wanaotumia dawa za kulevya Tanzania (TaNPUD), umeomba Serikali iwachukulie hatua  watu wanaochukua sheria mkononi dhidi ya watumia dawa za kulevya kwa kuwaona wao ni wahalifu na hawafai kwenye jamii.
Kauli hiyo ilitolewa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa mtandao huo, Godfrey Ten alipokuwa akizungumzia taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika kuhusu Utawala Bora.
Ten alisema taarifa hiyo inaonesha Tanzania ni nchi ya 102 kati ya nchi 175 duniani zinazoongoza kwa wananchi wake kujichukuliwa sheria mkononi.
Alisema kwa upande wa watumia dawa za kulevya nchini, wamekuwa wakiathirika zaidi kwa kuchukuliwa hatua na viongozi au baadhi ya vyombo vya sheria wakiwemo askari Polisi kwa kuwadhania wao ni wahalifu, na hawafai katika jamii.
"Tunaomba Serikali iangalie hili kwani tunanyanyaswa na polisi wanadhani watumiaji wa dawa za kulevya wote ni wahalifu, wamefanya hata katika jamii tuonekane hatufai," alisema Ten.
Alisema wahalifu wanaweza kuwa watu wa aina yeyote bila kujali anatumia dawa za kulevya au la  na kusema vitendo vya askari Polisi kuwaona ni wahalifu vinachangia wananchi nao kuwaona hawafai na hivyo kuchukua hatua mkononi wanapopita.
Ten aliongeza kuchukua hatua mkononi sio tu kwa kundi hilo bali pia sio vyema  kwa makundi mengine kama vile ya wazee, watu wenye ulemavu wa ngozi na makundi mengine.
Ofisa Sheria wa Shirika la Kimataifa la Madaktari wa
Ulimwengu  (MDM), Lina Saguti,  alisema vitendo vya kuchukua sheria mkononi vimekithiri na matukio hayo yanahitaji ufahamu zaidi wa hali na mahitaji ya watu wanaotumia dawa za kulevya.
Alisema MDM kupitia mpango wa kupunguza madhara kwa watumia dawa za kulevya, umefanikiwa kuwasaidia waathirika wa dawa hizo nchini kwa kuwaelimisha na kusaidia kupunguza matumizi ya dawa hizo.
" MDM tunafanya kazi kwenye nchi mbalimbali duniani, tunasaidia zaidi makundi ya watu walioathirika na njaa, dawa za kulevya, majanga ya asili, vita, magonjwa hata wale waliotengwa na jamii kwa sababu mbalimbali", alisema Saguti.
Kuhusu kuelimisha umma na jamii kwa ujumla jinsi ya kuwasaidia watu wanaotumia dawa za kulevya, Saguti alisema mafunzo kwa maofisa Polisi zaidi ya 1,800  na wahudumu wa afya 300 wametolewa nchini.
Alisema lengo ni jamii nzima kutambua jinsi ya kuwahudumia waathirika hao ambao wengi wao baada ya kuelimishwa na kupata tiba ya methadone wamepunguza ulevi huo na wengine wameacha na kurejea kwenye hali yao ya kawaida.

No comments: