SHULE YAZAWADIA WALIMU KWA KUFAULISHA

Bodi ya Shule ya Sekondari ya Gongo la Mboto iliyopo Ulongoni B katika Manispaa ya  Ilala, imetoa zaidi ya Sh milioni 2.8 kwa walimu wa shule hiyo , kama motisha baada ya  kufaulisha vizuri wanafunzi wa kidato cha nne kwa mwaka 2013.
Fedha hizo zimepatikana kutokana na msukumo mkubwa wa Mwenyekiti wa Bodi wa shule hiyo, inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Octavian Mshiu na  wajumbe wake.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi fedha hizo kwa walimu nane wa shule hiyo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mshiu alisema  hatua hiyo imelenga kuongeza morali ya ufundishaji shuleni hapo ili kuendelea kuleta matokeo mazuri kwa wanafunzi.
Alisema ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne kwa mwaka jana, umekuwa mzuri tofauti na miaka mingine ya nyuma, jambo lililowafanya kuvutiwa nalo na hivyo kuwapongeza walimu hao kwa kazi nzuri waliyoifanya.
"Tumeona vyema kuwapa motisha walimu kutokana na kazi nzuri waliyofanya, sisi kama bodi tumevutiwa na matokeo hayo hatua iliyotufanya tuchukue uamuzi huo,” alisema Mshiu.
Aliwaomba wadau mbalimbali na uongozi wa CCM kupitia jumuiya  zake, kujitokeza kusaidia kuwalipia ada wanafunzi wasio na uwezo ili waweze kujiunga na shule hiyo yenye idadi ndogo ya wanafunzi.
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Lugano Mwafongo alisema ufaulu huo ni hatua kubwa kwa shule hiyo na CCM kwa ujumla hivyo aliwataka wanafunzi, walezi na wazazi kuendelea kushirikiana ili shule hiyo izidi kupiga hatua zaidi kitaaluma.
Mkuu wa Shule hiyo, Mihambo Charles alisema motisha hiyo waliyopata itazidi kuongeza hali ya ufundishaji  kwa walimu. Alitaja walimu waliopata motisha hiyo kuwa ni Misiuzo Makungu aliyepata Sh 320,000, Huruma Mgonde Sh 280,000 na Samuel Ikuna aliyepata Sh 100,000.
Wengine waliopata motisha hiyo ni Mwalimu Jacob Ngalya Sh 240,000, Asia Ismail Sh 900,000, David Jackson Sh 360,000, Marwa Bisendo Sh 360,000 na Mkuu wa shule hiyo, Mihambo Charles Sh 200,000.

No comments: