PADRI AHOJI MAADILI YA UKAWA KWA WAASISI WA TAIFA

Hatua ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kukashifu Waasisi wa Muungano, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume, imezidi kubomoa vyama vinavyounda umoja huo kwa wananchi.
Hali hiyo imejitokeza jana wakati wa misa ya Pasaka katika makanisa mbalimbali, ambapo wahubiri walijikuta wakilazimika kukemea tabia ya viongozi wa Ukawa na wajumbe wengine wa Bunge Maalumu la Katiba ambao si wa Ukawa kutokana na vitendo vyao bungeni.
Katika Ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Dar es Salaam jana, Padri Edwin Kigomba, alizungumzia mmomonyoko wa maadili unavyozidi kuporomoka nchini kiasi cha waasisi wa Taifa kukashifiwa hadharani.
Akizungumzia Bunge Maalumu la Katiba, Padri Kigomba alisema baadhi ya viongozi wamejikuta wakitawaliwa na lugha za matusi, kebehi na kashfa jambo linaloonesha wazi mmomonyoko wa maadili unavyozidi kuporomoka nchini.
Alisema Yesu Kristo ni mfano wa kuigwa na watu wote kwani alisimamia vizuri maadili, lakini kwa sasa watu wanashindwa kuvumiliana na kuheshimu viongozi wetu jambo ambalo linaonekana wazi kwa viongozi wa dini na wa Serikali.
Padri Kigomba alisema jambo baya zaidi mpaka sasa hakuna mtu ambaye amejitokeza na kuwaziba mdomo watu wanaofanya vitendo hivyo, na kuonya ikiwa hatatokea kabisa, basi Tanzania haitaweza kuwa salama kwani wananchi hawataweza kulima wala kufanya shughuli nyigine kutokana na kila mmoja  kuwa na nguvu na uamuzi.
Katika misa iliyofanyika katika Kanisa la Uamsho
Pentecostal Mission of Tanzania (UPMT) Dodoma mjini, Makamu Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Living Mwambapa  alisema, uamuzi waliofikia Ukawa wa kutaka kufanya ziara na maandamano nchi mzima, inadhihirisha kuwa wameishiwa kisiasa.
Mbali na kuishiwa kisiasa, Askofu huyo alisema hali hiyo pia inaonesha Umoja huo unataka kutengeneza Katiba yao inayosimamia itikadi za vyama vyao vya kisiasa.
Alisema Katiba haitapatikana kwa njia za kususia vikao na kufanya maandamano, bali ni kwa kukaa pamoja na kutafuta jawabu wanaloweza kulipata.
Akizungumza Muungano, aliwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba iwapo wataona suala la Muungano linawachukulia muda mrefu, waliache na kuendelea kujadili vifungu vingine vya rasimu hiyo ya Katiba.
‘’Kama wakiona suala la Muungano linawachukulia muda mrefu wa kujadili ni vema waliache kwanza badala ya kujadili na waendelee na vifungu vingine vya rasimu,’’ alisema.
Aliwataka waumini wa Kanisa hilo kutojihusisha na ushabiki wa vyama vya siasa katika kipindi hiki ambacho rasimu ya Katiba mpya inajadiliwa na Bunge Maalumu.
Aliwataka kutumia nafasi kubwa katika kuombea kikao hicho kwa kuwa ndiyo kazi yao wanayotakiwa kuifanya na siyo kushabikia.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Pentecoste Holiness Association Mission (PHAM) Kanda ya Kati, Julius Bundala amewataka Watanzania kuwa kitu kimoja katika kipindi hiki ambacho wajumbe wa    Bunge Maalumu la Katiba wameonesha njia ya kutengana katika harakati za kutafuta Katiba mpya.
Askofu huyo ambaye alikuwa akihubiri katika Ibada ya Pasaka, alisema wakati wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakionesha malengo yao ya kiitikadi kichama, Watanzania kwa upande wao walitakiwa kuomba kwa nguvu zote ili Mungu awarudishe meza moja na nchi ipate Katiba yake iliyoboreshwa.
Aliwataka wajumbe wa Ukawa warudi kwenye mawazo ya pamoja ya kutunga Katiba ya Wananchi, badala ya kuendelea kung’ang’ania itikadi za vyama vya siasa ambazo hazikubaliki ndani ya mchakato huo wa kujadili rasimu ya Katiba mpya.
Mkoani Iringa, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk Owdenburg Mdegela alisema wajumbe wa Ukawa, hawawatendei haki Watanzania akiwemo yeye kwa kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Akiongoza ibada ya Pasaka katika Kanisa Kuu la Dayosisi hiyo mjini Iringa, Askofu Mdegela aliwataka wabunge hao ama
kurudi bungeni mara moja au watangaze kujiuzulu ujumbe wa Bunge hilo ili Serikali ijue njia nyingine ya kufanya kuwasaidia Watanzania kupata Katiba bora.
Alisema kwa kususia vikao vya Bunge hilo, wabunge hao hawajatenda haki kwasababu walipaswa kukabiliana na malalamiko waliyonayo kwa kutumia kanuni walizotunga wao wenyewe.
Dk Mdegela alisema kama wanaendelea na msimamo wa kususia Bunge hilo ni vyema warudishe kodi za wananchi walizolipwa kama posho.
“Tumesikia kwamba wamelipwa posho, kama ukweli ni huo na wao hawataki kurudi bungeni ni vyema wakajiuzulu na kurejesha posho walizopewa.
“Mwenendo wa Bunge hauridhishi; lugha zinazotumiwa hazifai kutumiwa katika chombo hicho muhimu kinachotegemewa kuwasaidia Watanzania kupata katiba wanayoitaka,” alisema.
Alimtaka mmoja wa wajumbe wa Ukawa anayetuhumiwa kutumia lugha zisizofaa kuwakejeli waasisi wa Muungano, kuomba radhi kwa Watanzania.
Ingawa hakumtaja jina, lakini mjumbe wa Ukawa anayetuhumiwa kuwakashifu waasisi wa Taifa, ni Tundu Lissu, ambaye amepewa cheo cha msemaji wa Ukawa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, alisema kauli zake zilitolewa kwa niaba ya umoja huo.
Lakini Askofu Mdegela alisema viongozi hao waliokashifiwa, Hayati Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume ni matokeo ya Muungano tulionao hivi sasa na ni chanzo cha amani, nuru na neema iliopo nchini.
Aliwataka Watanzania kutoichezea amani iliyopo nchini huku akikumbusha uvunjifu wa amani uliopoteza maisha ya watu wengi katika nchi jirani za Kenya, Rwanda na Burundi.
 Katika kulinda amani ya nchi, Askofu Mdegela aliisihi Serikali kuacha kutumia nguvu kubwa ya vyombo vya dola kwa sababu inaweza kuhatarisha zaidi amani iliyopo.
Kuhusu muundo wa Serikali, Dk Mdegela alisema; “binafsi naona muundo wa serikali tatu utawagawa Watanzania; napendekeza kama mfumo wa serikali mbili haufai basi ni bora tuwe na serikali moja.”
Alisema serikali tatu zinaweza kuongeza chuki miongoni mwa pande mbili za Muungano, Tanzania bara na Zanzibar.
“Serikali tatu inaweza kuwa mwanzo wa kusambaratisha nchi na baadaye tukajikuta upande fulani wa nchi unahitaji serikali nyingine,” alisema.
Akizungumzia changamoto ya Zanzibar katika mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya alisema, hoja ya Katiba ya Zanzibar, madaraka ya Rais wake na bendera yanaweza kujadilika kwa njia nyingine.
Naye Askofu  Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa, ameelezea kusikitishwa na kashfa, matusi na kejeli zinazotolewa na baadhi wa wajumbe wa  Bunge Maalumu la Katiba dhidi ya wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kutaka Bunge hilo
kuvunjwa kama hakuna jambo la msingi la kujadiliwa.
Akitoa salamu za Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam jana, Askofu Mokiwa  alisema  haoni sababu yoyote ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kushambuliwa kwa maneno mabaya, wakati imefanya kazi nzuri na nzito ya kukusanya maoni ya wananchi.
Alisema matusi na dharau zinazotolewa kwa Tume hiyo iliyokuwa chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Jaji Joseph Warioba, hayalengi kwa Tume hiyo peke yake bali kwa wananchi wote kwa kuwa Tume hiyo inawakilisha mawazo yaliyotolewa na wananchi wote.
“Tume ya Katiba ilikusanya ‘vichwa’ na ilifanya kazi nzuri kwa kutembea maeneo mbalimbali kuzungumza na wananchi, leo tunasikitika kusikia Tume inaambiwa imefanya vibaya na kufikia mahali hadi inatukanwa kabisa,” alisema Mokiwa.

No comments: