WANAFUNZI WA GOBA WAFARIKI WAKIOGELEA BWAWANI

Wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Goba, wamekufa baada ya kuzama wakati wakiogelea katika dimbwi la maji ya mvua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema wanafunzi hao ni Frank Charles (11) na Videson Peter (11).  Alisema walifikwa na mauti juzi saa 5:00 asubuhi katika maeneo ya Goba.
Alisema wakati wanaogelea katika dimbwi hilo, maji yaliwazidi nguvu na kuzama na miili yao iliopolewa na wakazi wa eneo hilo na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi.
Katika tukio jingine, Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Wanamaji Kigamboni, Emmanuel Kamugisha anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 na 25 amekufa baada  kugongwa na gari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo alisema ajali hiyo ilitokea Aprili 19 mwaka huu katika Barabara ya Kilwa  eneo la mzunguko wa Mgulani.
Alisema gari lenye namba za usajili T 141 CVJ, aina ya Dong Fen, lililokuwa likiendeshwa na Athumani Kibula (48), mkazi wa Morogoro akitokea Mivinjeni kuelekea Keko, alipokuwa akizunguka aligongana na pikipiki namba T 428 CKU aina ya Fekon na kusababisha kifo cha askari.
Alisema pikipiki hiyo ilikuwa ikiendeshwa na askari wa JWTZ, Florian Kamugisha akiwa na abiria wake, Emmauel Kamugisha ambaye pia ni askari wa JWTZ.
Alisema askari hao walikuwa wakitokea taa za kuongozea magari za Uhasibu kuelekea Mivinjeni. Katika ajali hiyo,  abiria Kamugisha alikufa papo hapo na dereva wake alipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema majeruhi amelazwa katika hospitali ya Lugalo na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo. Dereva wa gari lililosababisha ajali hiyo amekamatwa na upelelezi unaendelea.

No comments: