MEYA CHADEMA AMDUNDA MGAMBO WA KIKE ARUSHA

Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Prosper Msofe, anadaiwa kumpiga mgambo wa kike na kusababisha alazwe katika Hospitali ya Levolosi.
Msofe ambaye ni Diwani wa Kata ya Daraja Mbili kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, alifanya kitendo hicho juzi kwa Mgambo Mary Mshana, alipokuwa akiamuru mgambo, kuacha kukamata mali za wafanyabiashara ndogo wakati wa Operesheni ya kusafisha Jiji.
Kwa sasa, Mary amelazwa katika Hospitali ya Levolosi, ambako ameshaongezwa chupa sita za maji kutokana na kipigo hicho.
Hata hivyo, alipohojiwa jana, Msofe alidai mgambo huyo ndiye aliyeanza kumshambulia na ndipo yeye akajibu mapigo.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongella, alisema hatua hiyo ya Msofe ni usaliti wa kutaka kujiona yeye ni kiongozi bora kwa wananchi.
Alidai hatua ya Msofe, kumpiga mgambo wa kike na kuhamasisha mamia ya machinga kwenda kuvamia Bohari ya Jiji, kwa lengo la kupora mali zilizokamatwa na mgambo na kuhifadhiwa katika bohari hiyo, ni usaliti na unaopaswa kulaaniwa.
Mongella alisema uamuzi wa kuliweka Jiji katika hali ya usafi na wafanyabiashara ndogo, kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria, ni wa Baraza la Madiwani na Msofe ni miongoni mwa madiwani waliopitisha uamuzi huo.
Alisema anasikitishwa kuona Msofe anakwenda kwa machinga, kupinga utekelezaji wa uamuzi waliokubaliana wote, na kuhamasisha watu kufanya fujo kupinga uamuzi wa Baraza la Madiwani na kibaya zaidi kwenda kupora mali katika Bohari.
Mkuu huyo wa Wilaya, aliwataka wakazi wa Jiji la Arusha na vitongoji vyake, kulaani kwa nguvu zote kitendo alichofanya  Msofe, kwani yeye ni kiongozi ambaye hakupaswa kuchukua sheria mkononi.
Alisema mgambo wa Jiji la Arusha, wanatekeleza majukumu yao ya kuondoa machinga na wale wa Soko Kuu, kwa kufuata sheria zilizowekwa na Baraza la Madiwani.
‘’Namshanga Naibu Meya kuwa msaliti wa uamuzi ya Baraza la Madiwani na kibaya zaidi kwa uamuzi wake wa kumpiga mgambo wa kike bila sababu za msingi.
‘’Kama huyo mgambo wa kike alifanya makosa, yeye ni kiongozi alipaswa kumshitaki kwa wakubwa zake na sio kumpiga na kumdhalilisha na kuamua kuhamasisha wananchi na kusema uongo kwao ili aonekane bora,” alidai Mongella
Alisisitiza kuwa Operesheni Usafi wa Jiji na hatua ya kuzuia machinga  kufanya biashara ovyo barabarani, ni za kudumu na sio za kubahatisha. Aliwataka machinga, kuacha kuwasikiliza wanasiasa, kwani watawaponza kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
Mongella aliwataka wanasiasa kuacha kuingilia kazi za kila siku za watendaji wa Jiji, kwani hiyo sio kazi yao.
Alisisitiza kuwa operesheni ya kuondoa machinga katikati ya Jiji, iko pale pale na itaendelea kwa kasi ya hali ya juu.
‘’Naomba wanasiasa wafanye kazi zao na watendaji wafanye kazi zao, bila kuingiliana, na wote wajue hakuna mwanasiasa aliye juu ya sheria. Hatutavumilia kuona wanasiasa wanaachwa  kudhalilisha watendaji.
 ’Kama kuna kasoro zinapaswa kuelezwa kupitia vikao na sio kuchukua sheria mkononi hiyo haitavumiliwa tena,‘’ alionya Mongella.
Akizungumzia tuhuma za kumpiga mgambo wa kike, Msofe alidai mgambo huyo ndiye aliyeanza kumshambulia na ndipo yeye alipojibu mapigo bila ya kusita.
Msofe alihoji kama yeye Naibu Meya amepigwa, iweje raia wa kawaida na kuongeza kuwa kutokana na hali hiyo, ametangaza vita kwa mgambo wote wa Jiji la Arusha kuanzia ofisini hadi majumbani kwao, kwamba watasakwa tu ili nao waadhibiwe.
Alisema wananchi wa Jiji la Arusha wamekuwa wakinyanyaswa  na mgambo walioko katika Operesheni, ikiwemo kupigwa kama wakimbizi, kunyang’anywa fedha na mali zao, hivyo yeye kama Naibu Meya hilo hatalivumiliwa kamwe na ameamua kutangaza vita hiyo.  
Alipoulizwa ni kwa nini hakulifikisha suala hilo la mgambo, kukiuka utaratibu katika vikao au kwa viongozi wao, alisema amekuwa akisema mara kwa mara katika vikao husika ili kupata majibu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Msofe alisema kutokana na hali hiyo ameamua yeye binafsi kwa kushirikiana na wananchi, ambao mali zao zimekamatwa, kuwasaka mgambo kila kona ya Jiji la Arusha kuanzia ofisini hadi majumbani kwao ili  waadhibiwe na kusikia machungu kama wengine.
Hata hivyo, akizungumza kwa uchungu na gazeti hili akiwa hospitalini
Levolosi, Mary alikanusha madai ya kumshambulia Naibu Meya, kwa maelezo kuwa   kamwe hawezi kumshambulia kwa namna yoyote ile.
Mary akisimulia mkasa huo, alidai Msofe alifika katika Bohari ya Jiji na vijana wengi ambao baadhi yao ni wafuasi wa Chadema na wengine ni  machinga, ambao mali zao zimekamatwa na walimkuta yeye akiwa zamu.
Alidai kuwa ghafla Msofe, alianza kuzungumza huku akitoa matusi ya nguoni na kuhoji mabosi wake wako wapi, kwani anataka mali zote zilizokamatwa na kuhifadhiwa humo ndani, ziachiwe.
Baada ya kuona hali inakuwa ngumu, Mary alidai alimuuliza Naibu Meya ni kwa nini ameamua kumtukana wakati yeye amekuwa akitekeleza uamuzi wa vikao vyao kuhusu usafi wa Jiji na uondoaji machinga mitaani.
Mary alidai kuwa alimshauri Naibu Meya kwenda kwa viongozi wake ili  apate maelekezo ya kuachia mali za machinga, tofauti na hapo ambapo hana uwezo wa kuachia chochote.
Mgambo huyo alidai baada ya kutoa ushauri huo,  ghafla alishikwa nguo yake ya kazi kifuani na kupigwa kibao na alianguka chini bila ya kujibu na kujipangusa lakini aliendea kumshambulia.
Mary alidai wakati akishambuliwa na Meya, kundi la vijana aliokuja nao, walikuwa wakimshangilia  na hakuwa na namna ya kufanya chochote,
zaidi ya kulia.
‘’Nimedhalilishwa sana bila kosa, siwezi kumpiga yule baba, kwanza ni mkubwa sana kimwili  na pili alikuwa na kundi kubwa sana la vijana… madai anayosema kuwa mimi nimempiga, sio ya kweli, anajitetea tu aseme ukweli,’’ alisema.

No comments: