NYALANDU ATAKA MOTISHA KATIKA VITA DHIDI YA UJANGILI...

Tembo, moja ya wanyama wanaolengwa sana na majangili.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amelitaka Baraza kuu la Wafanyakazi la Wizara, kuandaa utaratibu wa kutoa motisha kwa kila mfanyakazi kwa ajili ya kufanikisha  utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Mkubwa Sasa (BRN), katika kupambana na vita dhidi ya ujangili na kuongeza mapato yatokanayo na utalii.

Nyalandu alisema hayo katika hotuba yake ya kufungua Baraza kuu la wafanyakazi wa wizara  hiyo jana, mjini hapa, na kusisitiza kuwa kuwapatia motisha wafanyakazi, kutasaidia  kuwapa morali ya kufanya kazi bila kuchoka hasa katika kipindi hiki cha serikali chini ya wizara hiyo kukabiliana na vita dhidi ya ujangili nchini.
Hata hivyo alisema katika vita dhidi ya ujangili ni lazima kila mfanyakazi wa wizara ashirikishwe kikamilifu kwa nafasi yake  ili kufanikisha ushindi, kwa ufanisi mkubwa na suala la kuwapatia motisha halikwepeki na kutaka Baraza kuweka  uzito katika  mipango ya bajeti ya Wizara.
Akizungumzia mipango mkakati wa kupambana na ujangili, Nyalandu alisema Serikali itaipatia vitendea kazi yakiwemo magari na kununua helikopta kadhaa zinazoweza kupambana kijeshi na zenye uwezo wa kufanya doria nyakati za usiku.
"Katika kupambana na vita dhidi ya ujangili, wizara tutapata helikopta zitakazowezesha kuendesha doria na kupambana kijeshi pia zina uwezo wa kufanya doria usiku," alisema Waziri huyo.
Waziri huyo bila kutaja idadi ya helikopta hizo, alisema kuwa mwezi Julai mwaka huu wanatarajia kuwafundisha marubani wa kuziendesha ili ziweze kutumika kwenye operesheni za kupambana na majangili.
"Operesheni ya pili ya Tokomeza inatarajia kuanza  hivi karibuni  na ili tuweze kufanikiwa  zaidi ni wajibu wa Baraza hili la Wafanyakazi kuweka motisha ili kila mmoja ashiriki kikamilifu kupambana na vita hivi ambavyo ni lazima serikali ishinde," alisema Nyalandu.
Mbali ya kuzungumzia vita dhidi ya ujangili, alilitaka pia Baraza kuu la Wafanyakazi kuangalia mifungo ya uendeshaji wa kitengo cha sheria na kukiwezesha katika kuendesha kesi ambazo mara nyingi wizara imekuwa ikishindwa kezi zake nyingi Mahakamani.
"Wapo watu wanaifanya Tanzania ni shamba la bibi katika suala la kesi za ujangili inaona Serikali kwa maana Wizara ikashinda ...ni moja tu ambapo juzi, Jaji ametoa hukumu kwa jangili kifungo cha miaka 20...binafsi yangu hukumu hii ilinifanya nisherehekee," alisema Waziri.
Katika hatua nyingine, amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kuuza magari mabovu yasiyofanya kazi na yanayotumia fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo ili fedha zitakazopatikana zitumike kwa majukumu mengine ndani ya Wizara, kwani kwa sasa imekuwa na mpango wa kununua magari mapya ya kuwezesha uendeshaji wa majukumu yake.

No comments: