UGONJWA WA HATARI WAZIDI KUITESA DAR, WATU 144 HOI...

Dk Donan Mmbando.
Wagonjwa 144 wamethibitika kuwa na ugonjwa wa homa ya Dengue hadi wiki iliyopita jijini Dar es Salaam huku mtu mmoja akifariki dunia.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donan Mmbando, Wilaya ya Kinondoni ndiyo inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa 132, Ilala ina wagonjwa wanane na Temeke wanne.
Alimtaja mgonjwa pekee aliyefariki dunia kutokana na ugonjwa huo ni mwanamke mwenye umri wa miaka 22 baada ya kutoka damu nyingi puani na sehemu za wazi.
Dk Mmbando alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya hali halisi ya ugonjwa huo hadi kufikia mwisho wa mwezi uliopita, ambapo katikati ya mwezi huo kulikuwa na wagonjwa 70.
Alisema Kata zilizoathirika na ugonjwa huo ni Mtoni, Tandika, Yombo, Mabibo, Sinza, Temeke, Mikocheni, Manzese na Msasani, ambapo wanawake walioathirika ni 64 na wanaume 80.
"Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa huu au chanjo kwa kinga kwa binadamu bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa kama homa, kupungukiwa maji au damu," alisema.
Dk Mmbando alitaja dalili kuu za ugonjwa huo kuwa ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu ambazo huanza kujitokeza kuanzia siku tatu hadi 14 tangu mtu anapoambukizwa kirusi hicho.
"Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinafanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanatakiwa kuwa waangalifu hasa wakati wakipata homa zinazofanana na malaria, lakini wakipimwa vimelea vya malaria havionekani," alisema.
Alisema ugonjwa huo si mpya nchini, kwani uligundulika kwa mara ya kwanza mnamo Juni 2010 mkoani humo na watu 40 waliothibitika kuwa na ugonjwa huo, huku kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huo na hakuna aliyepoteza maisha.

No comments: