NDEGE ZILIZOACHWA NA NYERERE BADO ZINAFANYA KAZI

Wakala wa Ndege za Serikali umesema  unajivunia kuwa na ndege  mbili zilizoachwa na Hayati  Mwalimu Julius Nyerere zinazohudumia viongozi wote wa Muungano hadi sasa.
Ofisa Masoko wa wakala huo, Monica George alisema hayo  mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na gazeti hili katika maonesho ya taasisi za Muungano ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.
Alisema ziliachwa kipindi cha uongozi wa Hayati Nyerere na kwamba zimekuwa zikitumika kwa kuhudumia viongozi wa awamu zote kwa upande wa bara na visiwani.
“Wakala umekuwa ukitoa huduma ya usafiri kwa viongozi wa wakuu wa kitaifa ambapo licha ya kuwa na ndege nne kwa sasa lakini tunajivunia kuwa na ndege mbili ambazo ziliachwa na Nyerere na bado ziko salama,” alisema Monica.
Alizitaja ndege hizo zilizoachwa kuwa ni Fokker 28 na Fokker 50 ambazo zinatumika kuhudumia viongozi hao wa Muungano ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Zanzibar, Makamu wa Rais  na Waziri Mkuu.
Alisema ndege aina ya Fokker 28 kwa sasa iko  Uholanzi kwa ajili ya matengenezo ya kawaida. Alisema ndiyo  ya kwanza kufungua safari za idara na kufika hadi Ulaya ambayo ilinunuliwa mwaka 1978.
Aidha alisema ndege aina ya Fokker 50 ilinunuliwa mwaka 1992 na  imekuwa ikitumika kwa safari za ndani na nje ya nchi.

No comments: