CHUO KIKUU INDIA KUWAKOMBOA VIJANA

Chuo Kikuu cha Rajendra Singh cha nchini India kimesema kipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuwapatia vijana elimu ya masuala ya kibiashara waweze kujiajiri na kuwaajiri wengine kupunguza tatizo la ajira nchini hususani kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Mkurugenzi wa Chuo hicho, Dk Sarit Kumar alisema jijini hapa jana kuwa kwa sasa chuo hicho kinatoa mafunzo ya namna hiyo katika nchi za Rwanda, Senegal na Ivory Coast na hivyo wameona umuhimu wa kuyaanzisha hapa nchini ili kukamilisha azma yao hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema chuo hicho pia kitakuwa kikiwasaidia vijana hao namna ya kupata mitaji ya kufanya biashara baada ya wataalamu wa biashara wa chuo hicho kujiridhisha na wazo la kibiashara atakalobuni mwanafunzi.
“Kimsingi chuo chetu ni moja ya vyuo vinavyoheshimika sana nchini India  kwakuwa kina wataalamu waliobobea katika masuala ya uchumi na biashara.
“Kutokana na uchumi wa Bara la Afrika kuanza kukua kwa kasi, tumekuwa tukitoa mafunzo kama haya kwa vijana wengi katika nchi za  Afrika na sasa tunataka vijana wa kitanzania nao waweze kunufaika na fursa za kiabiashara walizonazo,” alisema.
Aidha Dk Kumar alisema uchumi na pato la mataifa ya Afrika unaweza kuimarika kama vijana wa kiafrika watapata mafunzo imara ya kibiashara ili biashara za Afrika zifanywe na vijana wenyewe wa kiafrika badala ya kutegemea mataifa ya kigeni.
Alisema lengo kuu la mpango huo ni kuwafanya vijana kutokuwa wategemezi na kwamba wamekuwa wakihakikisha vijana wanaosoma masomo hayo ya biashara wanapatiwa mitaji na hatimaye kujiendesha wenyewe na kuchangia pato la Taifa.
Juresh Babra, ambaye ni miongoni mwa maofisa wa chuo hicho aliwataka Watanzania kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo ya masomo ambayo itawasaidia kupata mbinu za kujikwamua na umasikini.

No comments: