MOTO WATEKETEZA MADUKA NA NYUMBA YA MBUNGE

Moto umezuka mjini Dodoma na kusababisha maafa katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba ya Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi iliyoteketea na mali mbalimbali.
Wakati  nyumba hiyo ya Mbunge na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT) iliteketea juzi saa 3 usiku, muda huo huo, moto mwingine umeteketeza nyumba ya biashara yenye maduka mengi katika eneo lililo mkabala na CCM makao makuu, mjini hapa.
Akizungumzia nyumba ya mbunge, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema wakati wa tukio hilo lililosababisha uharibifu mkubwa wa mali,  Makilagi alikuwa safarini.
Alisema thamani ya mali iliyoteketea na chanzo cha moto huo hakijafahamika na Polisi inaendelea na uchunguzi.
Kuhusu maduka yaliyoteketea, Kamanda alisema pia juzi saa 2:30 usiku,  katika mtaa wa Barabara ya Nyerere  nyumba ya biashara yenye maduka mengi iliungua na kuteketeza bidhaa katika maduka yapatayo manne.
Miongoni mwa walioathirika na moto huo, ni mkazi wa Ipagala,  Frank Pilla (45)  ambaye licha ya duka lake lijulikanalo kama Mahavaz Gumo lenye bidhaa za chakula kuteketea, yeye pia alijeruhiwa kwa moto sehemu za mikononi na usoni.
Alikimbizwa Hospitali ya Mkoa Dodoma ambako alipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Maduka mengine yaliyoteketea ni la vifaa vya maofisini na shuleni  na M-Pesa linalomilikiwa na Esheki Moshi (54) mkazi wa Miyuji.
Mengine ni  duka la vipodozi la Malaika linalomilikiwa na Jamila Baduwel (30) mkazi wa Area ‘D’ na duka la dawa baridi la Kavula linalomikiwa na  Mariam Rashidi (40) mkazi wa Chamwino.
Kamanda Misime alisema moto ulianzia katika duka la Mahavaz Gumo na kusambaa kwa kasi katika maduka mengine ya jirani na kuteketeza mali zilizokuwemo.
Alisema thamani ya mali iliyoteketea haijafahamika na chanzo cha moto huo hakijafahamika huku uchunguzi unaendelea.

No comments: