MVUA YABOMOA NYUMBA 300 RORYA

Nyumba 300 katika kata tano wilayani Rorya, zimeharibiwa na mvua iliyonyesha mwishoni mwa wiki.
Sambamba na uharibifu huo, mvua hiyo pia imeharibu ekari 500 za mazao ya mahindi, mtama, muhogo na migomba.
Uharibifu huo umetokea kwenye kata za Ikoma , Koryo , Bukura, Nyahongo na Mkoma.
Taarifa hizo zilitolewa kwa nyakati  tofauti  jana na madiwani wa kata hizo, Laurent Adrian wa Ikoma, Musa Ago wa Nyahongo na  Pendo Odele wa Viti Maalumu.
Madiwani hao walisema mvua hiyo, iliyoambatana na upepo mkali, ilianza kunyesha saa 11:00 jioni Aprili 13, mwaka huu na kuezua mabati kwenye nyumba 140. Nyumba 163 za nyasi nazo ziliharibiwa.
Ago alisema "kwa sasa zaidi ya kaya 150 hazina makazi na zimejihifadhi kwa ndugu zao na hazina chakula".
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya,  Samwel Kiboye alisema  " CCM tunajiandaa kusaidia kaya na familia zilizokumbwa na maafa hayo, kutokana na nyumba zao na mazao kuharibiwa vibaya na mvua hizo".
Mbunge wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo alihidi kutoa misaada kwa familia, zilizoathiriwa na mvua hiyo.
Mkuu wa Wilaya hiyo,  Elias Goroi hakupatikana kuzungumzia suala hilo la maafa ili kujua Serikali imejipanga vipi kusaidia familia hizo.

No comments: