NDEJEMBI ATAKA VIJANA NA WAZEE KUJIKITIKA KWENYE KILIMO

Wazee wastaafu na vijana wametakiwa kuelekeza nguvu kwenye sekta ya kilimo ili waweze kujiajiri wenyewe, kwani  ndio ukombozi wa maisha.
Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pancras Ndejembi alisema hayo juzi wakati akikabidhi  mkopo wa matrekta kwa wakulima,  yaliyotolewa na Kampuni ya NAM LTD ya mjini hapa.
Alisema kilimo ni sekta muhimu kwenye ajira  ya  maisha na itasaidia jamii kuendesha maisha  yao  kila siku na kwenye biashara.
Ndejembi alisema wakulima wakiwezeshwa mikopo ya  zana za kilimo, kama matrekta wanaweza kujikwamua kiuchumi na kufanikisha kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na viongozi  bila kuwa na mafanikio makubwa.
Mkulima Idd Simbai, Mwalimu mstaafu kutoka Wilaya ya Kondoa mkoani hapa, aliishauri  Kampuni ya NAM Ltd kuwasaidia mikopo ya matrekta, kwani wasingeweza kununua kwa pesa  taslimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NAM Ltd,  Aspenance Ng'aranga, alisema kampuni hiyo inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima ili kuwawezesha kuondokana na kutegemea kilimo cha jembe la mkono.
Alisema kampuni yao, inawakopesha wakulima kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kwa kudhaminiwa na halmashauri zao na kwa kujidhamini wenyewe.
Aidha, alisema wanaendelea kuwakumbusha wakulima wale waliokopeshwa kuendelea kujenga uaminifu kwao kwa kuendelea kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.

No comments: