MVUA SASA KUNYESHA KWA WASTANI

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imesema  mvua zitakazoendelea kunyesha kwa sasa ni za kiasi.
Wakati TMA ikitoa taarifa hiyo jana, usafiri wa mabasi yaendayo mikoani kutoka jijini Dar es Salaam jana uliendelea kuwa mgumu.
Mkurugenzi wa TMA, Dk Agnes Kijazi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema mamlaka inaendelea kufuatilia kuona kama kuna mabadiliko mengine ya hali ya hewa.
"Ile tahadhari yetu ya mvua kubwa imeishia leo (jana) lakini bado Mamlaka inaendelea kufuatilia kuona kama kuna mabadiliko mengine ya hali ya hewa," alisema Dk Kijazi na kuongeza katika mfumo wa hali ya hewa kuna mfumo unaoonekana ingawaje ni mapema  kutoa taarifa.
Kuhusu usafiri,  Mkuu wa Kituo cha Usalama Barabarani Ubungo, Mkaguzi wa polisi, Yusuf Kamotta alisema jana hadi saa 7:00 mchana hakuna mabasi yaliyoruhusiwa kutoa huduma kutokana na hali ya daraja la Ruvu.
Hata hivyo, Kamanda wa Kikosi ch Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema daraja la Ruvu liko imara isipokuwa tatizo lilijitokeza meta kati ya 50 na 100 kutoka darajani ambako udongo ulilika chini ya lami.
"Tanroads na wataalamu wengine wako pale wakiweka mawe ili pawe imara ili kuruhusu magariÉhadi saa 8 (jana) nilivyoongea nao walikuwa wakimalizia kazi hiyo," alisema na kusisitiza pakiwa salama, ataruhusu magari yote. 
Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alisema wakulima 17 waliokolewa juzi mashambani baada ya kukumbwa na mafuriko eneo la Mtoni jirani na Bagamoyo mjini kwenye barabara ya Msata - Bagamoyo.
Pia mwili wa mtu anayedhaniwa kuwa mkazi wa Muheza wilayani Kibaha ukikadiriwa kuwa na umri wa miaka 36,  umekutwa ukielea kwenye mto Mpiji baada ya kupotea kwa siku tatu zilizopita.

No comments: